

Lugha Nyingine
Mienendo ya hali ya ghasia inaendelea katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu: Mjumbe wa Umoja wa Mataifa (2)
![]() |
Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati Tor Wennesland (kwenye skrini) akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Agosti 21, 2023. (Loey Felipe/Picha ya UN/ Xinhua) |
UMOJA WA MATAIFA – Mienendo ya hali ya ghasia zilizoshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni inaendelea katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati Tor Wennesland amesema Jumatatu, huku akisisitiza haja ya kurejesha upeo wa kisiasa na kufikia suluhu ya kuunda nchi mbili.
“Wapalestina na Waisraeli wanauawa na kujeruhiwa katika ghasia zinazokaribia kutokea kila siku ambazo huchochewa na kuongezwa zaidi na hali inayoongezeka ya kukata tamaa kuhusu siku zijazo,” Wennesland amesema katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama.
Amesema, ghasia zinaendelea kuongezeka, huku Wapalestina zaidi ya 200 na Waisrael karibu 30 wakiwa wameuawa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Israel hadi sasa mwaka huu, ikiwa tayari imepita takwimu za Mwaka 2022, na ni idadi kubwa zaidi tangu Mwaka 2005.
Upanuzi wa makazi unaendelea bila kusitishwa, Wennesland amesema, huku akiongeza kuwa hali tete ya kifedha ya Mamlaka ya Palestina, ikijumuishwa na uhaba wa fedha unaokabili mashirika muhimu ya Umoja wa Mataifa, inatishia kuzidisha hali mbaya ya Wapalestina walio hatarini zaidi.
"Ingawa ni lazima tujikite kwa haraka kushughulikia masuala muhimu zaidi na kupunguza hali ya ghasia mitaani, hatuwezi kupuuza haja ya kurejesha upeo wa kisiasa," amesisitiza.
Wennesland amesema kwamba, Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa na nia thabiti ya kuunga mkono pande hizo ili kufikia mwisho wa ukaliaji kwa mabavu ardhi ya Wapalestina na kufikiwa kwa suluhu ya kuunda nchi mbili, kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya hapo awali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma