Marais wa China na Afrika Kusini wakutana na wanahabari baada ya mazungumzo

(CRI Online) Agosti 23, 2023
Marais wa China na Afrika Kusini wakutana na wanahabari baada ya mazungumzo
(Picha inatoka Xinhua.)

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wamekutana na waandishi wa habari kwa pamoja baada ya mazungumzo .

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Jumanne, Agosti 22, Rais Xi amesema, huu ni mwaka wa 25 tangu uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika Kusini ulipoanzishwa. Katika miaka 25 iliyopita uhusiano huo umepiga hatua kubwa, huku hali ya kuaminiana kimkakati kati ya pande hizo mbili ikifikia kiwango kipya cha juu.

Amesemea, Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye nyanja mbalimbali umeendelea kusonga mbele, haswa kwenye mifumo ya uhusiano wa pande nyingi. Amesema, uhusiano kati ya China na Afrika Kusini umevuka mipaka ya pande mbili, na kuzidi kuwa na umuhimu wa kimkakati na ushawishi wa kimataifa.

Rais Xi amesema yeye na mwenzake Ramaphosa wamefikia makubaliano mengi kwenye mazungumzo yao, na wamebadilishana maoni kuhusu maendeleo ya uhusiano wa pande mbili katika zama mpya na masuala ya kikanda na kimataifa yanayofuatiliwa kwa pamoja. Pia wameshuhudia kusainiwa kwa nyaraka mbalimbali za ushirikiano wa pande mbili. Rais Xi amesema ana imani na mustakabali wa uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika Kusini.

Rais Xi amesema wamekubaliana kuwa China na Afrika Kusini zitaendelea kuwa wenzi wa maendeleo ya pamoja, zikiendelea kuunganisha mikakati yao ya maendeleo, na kuimarisha na kupanua zaidi ushirikiano uliopo wakati wa kutekeleza Miradi Tisa ya FOCAC na Mpango wa Ushirikiano wa Kimkakati wa Miaka Kumi kati ya China na Afrika Kusini.

Rais Xi amesema China na Afrika Kusini zote ni nchi zinazoendelea zenye ushawishi mkubwa na masoko mapya yanayoibuka, na pande hizo mbili zinapaswa kuwa wenzi wa kulinda haki duniani.

Rais Xi amesisitiza kuwa yeye na mwenzake Ramaphosa wataongoza kwa pamoja mazungumzo kati ya viongozi wa China na nchi za Afrika, ambao ni ya kwanza tangu kutokea kwa janga la UVIKO-19 Mwaka 2019. Wanatarajia kufanya kazi pamoja na viongozi wengine watakaoshiriki kwenye mkutano huo, kuweka dira mpya kwa mshikamano na ushirikiano kati ya China na Afirka na kutoa msukumo mpya kwa maendeleo ya uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Afrika.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amesema, watu wa Afrika Kusini wanaishukuru serikali na wananchi waChina kwa kuiunga nchi yao kwenye mapigano dhidi ya ubaguzi wa rangi na maendeleo ya taifa, na vilevile kutoa misaada mingi ya vifaa tiba kwa Afrika Kusini wakati wa janga la UVIKO-19.

Rais Ramaphosa amesema, yeye na Rais Xi wamesisitiza tena kuwa nchi zao zitaendelea kuungana mkono kwenye maslahi makuu ya kila upande na masuala makubwa yanayofuatiliwa kwa pamoja. Pia wamekubaliana kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana kwenye nyanja mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu, utalii, elimu na uchumi wa kidijitali, na kuimarisha uratibu kwenye masuala makubwa ya kikanda na kimataifa.

Rais Ramaphosa amesema anatarajia kushirikiana na Rais Xi na viongozi wengine wa BRICS katika kuongeza sauti za BRICS na nchi za Ulimwengu wa Kusini kwenye uongozi wa dunia, na kusukuma mbele ujenzi wa utaratibu wa kimataifa ulio wa haki zaidi. Rais Ramaphosa pia anatarajia kuongoza mazungumzo kati ya viongozi wa China na Afrika pamoja na Rais Xi, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na China.

Amesema, anaamini kuwa mazungumzo hayo yatasaidia kusukuma mbele maendeleo ya viwanda na muunganisho wa kikanda barani Afrika, na pia kuchangia maendeleo na ustawi wa pamoja wa nchi za Ulimwengu wa Kusini.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha