Spika wa Bunge la China atoa wito wa kuimarisha mabadilishano na Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 29, 2023
Spika wa Bunge la China atoa wito wa kuimarisha mabadilishano na Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Zhao Leji, Spika wa Bunge la Umma la China akifanya mazungumzo na Adel Al Asoomi, Spika wa Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma hapa Beijing, China, Agosti 28, 2023. (Xinhua /Liu Bin)

Beijing – Spika wa Bunge la Umma la China Zhao Leji amefanya mazungumzo na Adel Al Asoomi, Spika wa Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, siku ya Jumatatu mjini Beijing, akitoa wito wa kuimarishwa kwa mabadilishano kati ya mabunge ya pande mbili.

Zhao amesema, chini ya mwongozo wa kimkakati wa viongozi wa China na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, uhusiano kati ya China na nchi za Kiarabu umepata maendeleo makubwa.

“China iko tayari kushirikiana na nchi za Kiarabu kutekeleza matokeo ya mkutano wa kwanza wa wakuu wa China na Nchi za Kiarabu, kuendeleza moyo wa urafiki kati ya China na nchi za Kiarabu unaojumuisha kusaidiana, usawa, kunufaishana, ushirikishi, na kufunzana, na kufanya juhudi ziwezavyo kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Nchi za Kiarabu katika zama mpya,” Zhao amesema.

Amebainisha kuwa pande hizo mbili zinapaswa kuendelea kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa na kuungana mkono kithabiti katika masuala yanayohusu masilahi ya msingi na mambo yanayofuatiliwa ya pande mbili, akisema China iko tayari kuzidisha ushirikiano wa kivitendo na nchi za Kiarabu na kuhimiza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja.

Ni matumaini kuwa pande hizo mbili zitatekeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi na kulinda kwa pamoja haki na usawa, Zhao amesema na kuongeza kuwa China iko tayari kufanya mabadilishano ya kitamaduni na nchi za Kiarabu, kutekeleza Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia, kupanua mabadilishano katika utamaduni, elimu na utalii, na kuimarisha uungaji mkono wa watu wengi kwa ushirikiano wa kirafiki.

Zhao amesema, kuanzishwa kwa utaratibu wa mabadilishano kati ya Bunge la China na Bunge la Nchi za Kiarabu kutaongeza msukumo mpya katika maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Adel Al Asoomi, huku akipongeza haja ya kuanzisha mabadilishano kati ya mabunge hayo mawili, amesema nchi za Kiarabu zinafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja na kuunga mkono Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia, na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia.

Baada ya mazungumzo hayo, Zhao na Adel Al Asoomi kwa pamoja walitia saini mkataba wa makubaliano ya kuanzisha utaratibu wa mabadilishano kati ya Bunge la China na Bunge la Nchi za Kiarabu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha