

Lugha Nyingine
Mkutano wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa wafunguliwa
UMOJA WA MATAIFA - Mkutano wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa umetangazwa kufunguliwa siku Jumanne na mwenyekiti mpya wa Baraza Kuu Dennis Francis.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano iliyosomwa kwa niaba yake na naibu wake, Amina Mohammed, ameonya juu ya Dunia ya changamoto kubwa na mgawanyiko ambao unauweka Umoja wa Mataifa majaribuni.
"Ingawa tunakabiliwa na changamoto kubwa za kimataifa, lakini huu siyo wakati wa kukata tamaa. Huu ni wakati wa kuchukua hatua," amesema. "Hatua ya amani na haki za binadamu; hatua ya kuokoa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kukabiliana na tishio lililopo la mabadiliko ya tabianchi; hatua ya kujitahidi kutoa nafasi za ajira za uzalishaji bidhaa na kupanua fursa za kiuchumi, haswa kwa wanawake na vijana; hatua ya kuhakikisha kuwa mageuzi ya haraka katika teknolojia kama akili bandia ni msaada, na si madhara, kwa binadamu; hatua ya kujenga Dunia yenye matumaini na fursa kwa wote ambayo haimwachi mtu yeyote nyuma."
"Zaidi ya jukwaa lolote duniani, Baraza Kuu linawakilisha ubinadamu wetu wa pamoja na dhamira yetu ya pamoja kwa ajili ya amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu. Hebu tutafute suluhu ambazo watu wote wanatarajia na kufanya maendeleo kuelekea siku za baadaye zenye maisha bora, amani na mafanikio zaidi, na sayari yenye manufaa zaidi," Guterres amesema.
Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mkutano, Francis amesema Baraza Kuu la awamu mpya limeanza" katika hali ambayo ajenda muhimu na zenye taabu kubwa za kimataifa zinakumbwa na mfululizo wa changamoto zinazoendelea."
Ametoa wito kwa nchi wanachama kusukuma na kudumisha amani kwa kuwawezesha wale walio katika mazingira hatarishi zaidi; kutoa ustawi wa pamoja kwa kufungua rasilimali zinazohitajika kwa matokeo ya mageuzi; kuharakisha maendeleo kwa kutumia nguvu ya msukumo waliyonayo vijana, uvumbuzi na teknolojia, ili kuhimiza uendelevu.
"Katika Baraza Kuu la awamu hii nitajitolea kushirikisha makundi ya kikanda na mengine ili kushirikiana kwa pamoja katika kuleta uhai mpya kwenye hali ya ushirikiano wa kimataifa na ahadi za pamoja. Matarajio yangu ni Baraza Kuu kushughulikia changamoto nyingi zinazolikabili kwa ufanisi na kwa njia jumuishi iwezekanavyo," Francis amesema.
Ametoa wito kwa nchi wanachama kutumia moyo wa ushirikiano wa kweli wa pande nyingi katika kutatua matatizo "ili tuweze kulinda vyema zaidi (kama siyo kuhakikisha) usalama na utu wa binadamu."
Francis, mwanadiplomasia kutoka Trinidad na Tob ago, aliapishwa kuwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la 78 wakati wa kufungwa kwa mkutano wa Baraza Kuu la 77 Jumanne asubuhi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma