Reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kikanda kuelekea maendeleo ya kisasa - Waziri Mkuu wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2023
Reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kikanda kuelekea maendeleo ya kisasa - Waziri Mkuu wa China
Waziri Mkuu wa China Li Qiang ambaye yuko ziarani nchini Indonesia, akifuatana na Mratibu wa Ushirikiano kati ya Indonesia na China na Waziri Mratibu wa Masuala ya Bahari na Uwekezaji Luhut Binsar Pandjaitan, akikagua Reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung nchini Indonesia, Septemba 6, 2023. (Xinhua/Rao Aimin)

JAKARTA - Reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung ni mfano mzuri wa nchi zinazoendelea katika kanda hiyo kushirikiana kutimiza maendeleo ya kisasa, Waziri Mkuu wa China Li Qiang amesema Jumatano wakati akikagua mradi huo wa ushirikiano kati ya China na Indonesia.

Alipowasili katika Stesheni ya Reli ya Halim, Waziri Mkuu Li alikaribishwa kwa furaha na wafanyakazi wa China na Indonesia. Alisikiliza ripoti ya ujenzi wa reli hiyo na kueleza jinsi anavyothamini kazi kubwa iliyofanywa na wafanyakazi wa nchi hizo mbili.

Huku akibainisha kuwa ikiwa ni reli ya kwanza ya mwendo kasi katika eneo la Asia ya Kusini Mashariki, Reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung ni mradi kinara wa ushirikiano kati ya China na Indonesia chini ya pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja unaoungwa mkono na Rais Xi Jinping wa China na Rais wa Indonesia Joko Widodo, Waziri Mkuu Li amesema kwamba pia unabeba matarajio ya watu wa Indonesia kwa maisha bora.

“Pande hizi mbili zinapaswa kutekeleza maafikiano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kufanya maandalizi makini, kuhakikisha reli hiyo kuzinduliwa na kuendeshwa kwa kiwango cha juu, na kutia msukumo mkubwa na wa kudumu katika kuifanya Indonesia na kanda hiyo kwa ujumla kuwa na maendeleo ya kisasa,” Waziri Mkuu Li amesema.

Kisha Waziri Mkuu Li alifanya safari ya majaribio na kukagua ujenzi wa jukwaa la abiria kushuka na kupanda treni katika Stesheni ya Karawang. Akiita reli hiyo ya mwendo kasi safari ya kuelekea muunganisho, uwazi na ustawi wa pamoja, Waziri Mkuu Li amesema kuwa siyo tu itapunguza muda wa safari kati ya miji, lakini pia itakuza ufanisi na uboreshaji wa muundo wa viwanda na kuwezesha maendeleo ya kiuchumi katika maeneo kando ya reli hiyo.

“China iko tayari kuchangia utaalamu wake uliokomaa na Indonesia, na kushirikiana kufanya kazi nzuri katika kuendeleza viwanda na kustawisha miji kupitia reli hii ya mwendo kasi,” Waziri Mkuu Li amesema.

Ikiunganisha Jakarta, mji mkuu wa Indonesia, na Bandung, mji wa nne kwa ukubwa nchini Indonesia, Reli ya Mwendo Kasi ya Jakarta-Bandung ina urefu wa kilomita 142 na ina kasi ya juu ya reli ya kilomita 350 kwa saa.

Ni mradi wa kwanza wa reli ya mwendo kasi inayotumia kikamilifu mifumo ya reli, teknolojia, na vipengele vya viwanda vya China katika nchi za nje.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha