G20 yapanua fursa za ushirikiano na maendeleo ya nchi za kusini baada ya AU kujiunga

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 11, 2023
G20 yapanua fursa za ushirikiano na maendeleo ya nchi za kusini baada ya AU kujiunga
Picha hii iliyopigwa Septemba 9, 2023 ikionyesha majengo ya makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Wang Guansen)

NEW DELHI - Baada ya kukubali Umoja wa Afrika (AU) kuwa mwanachama wa kudumu, Kundi la nchi 20 (G20) limechukua hatua ya kihistoria katika kuboresha usimanizi wa kimataifa na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa.

Upanuzi huo, uliokubaliwa na pande wanachama wa G20 siku ya Jumamosi, unazipa nchi zinazoendelea sauti kubwa na uwakilishi zaidi. Ushirikiano na fursa zaidi za maendeleo zitaongezeka kuelekea nchi za Kusini kwani China na nchi nyingine zenye uchumi mkubwa zimeahidi kuunga mkono kwa dhati eneo hilo kuangaza katika jukwaa la kimataifa.

Kuchukua kiti

Huku kukiwa na shangwe na makofi kutoka kwa viongozi wa kimataifa waliohudhuria mkutano huo, Mwenyekiti wa zamu wa AU ambaye pia ni Rais wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani, alichukua kiti chake akiwakilisha chombo hicho cha Bara la Afrika chenye nchi wanachama 55 katika kikao cha ufunguzi wa mkutano wa 18 wa kilele wa G20 uliofanyika New Delhi siku ya Jumamosi.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki amepongeza kuingia huko kwa AU, akisema kutaongeza utetezi na michango ya Bara la Afrika kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Kundi la nchi 20 (G20), lililoanzishwa Mwaka 1999 kwa lengo la kukabiliana na misukosuko kadhaa ya kiuchumi duniani, ni jukwaa kubwa la kujadili masuala ya kifedha na kiuchumi. Hapo awali lilijumuisha nchi 19 pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).

Kuweka mazingira mazuri

Mathapelo Monaisa, mmoja wa maafisa wa ujumbe wa Afrika Kusini kwenye mkutano wa G20, ameshukuru mchango wa China katika kuunga mkono AU kujiunga katika kundi hilo. "Ninaona kitu kikubwa kinatokea," Monaisa amesema.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema China ilikuwa nchi ya kwanza kueleza wazi kuunga mkono AU kujiunga kwenye G20.

"China daima imekuwa ikitoa heshima, pongezi na uungaji mkono kwa Afrika, na watu wa China wamechangia misaada ya hali na mali na watu wa Afrika," amesema Joseph Matthews, profesa mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Beltei huko Phnom Pen, Cambodia.

Kujibu wito

Nchi nyingi zimekaribisha AU kujiunga katika G20, zikisisitiza uungaji mkono wao wa muda mrefu katika kuimarisha sauti ya Afrika, ikiwemo Uturuki ambayo wizara yake ya mambo ya nje imesema hatua hiyo "inawakilisha hatua muhimu ya kuenea kwa ushirikiano wa pande nyingi wenye ufanisi katika uhusiano wa kimataifa."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha