Waathirika zaidi ya 1,000 bado hawajatambuliwa miaka 22 baada ya tukio la mashambulizi ya kigaidi ya 9/11

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 12, 2023
Waathirika zaidi ya 1,000 bado hawajatambuliwa miaka 22 baada ya tukio la mashambulizi ya kigaidi ya 9/11
Watu wakihudhuria shughuli ya kumbukumbu ya kutimia miaka 22 tangu kutokea mashambulizi ya kigaidi ya 9/11 huko New York, Marekani, Septemba 11, 2023. Shughuli ya kumbukumbu imefanyika hapa Jumatatu kukumbuka kutimia miaka 22 tangu kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi ya 9/11. (Picha na Michael Nagle/Xinhua)

NEW YORK - Waathirika zaidi ya 1,000 bado hawajatambuliwa huku Marekani siku ya Jumatatu ikiadhimisha miaka 22 tangu kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11.

Shughuli ya kumbukumbu imefanyika Jumatatu kwenye Makumbusho ya Kitaifa ya Septemba 11 huko Lower Manhattan, New York, ambapo watu 2,977 waliofariki katika mashambulizi ya Septemba 11, 2001 walipewa heshima.

Siku chache kabla ya siku hiyo, utambuzi wa waathiriwa wawili wa shambulizi hilo baya zaidi la kigaidi kuwa kutokea nchini Marekani wametangazwa, mwanamume na mwanamke ambao majina yao yamehifadhiwa kwa ombi la familia zao.

Utambuzi huo mpya wa watu wawili unawakilisha watu 1,648 na 1,649 waliotambuliwa tangu Mwaka 2001 kwa kutumia uchunguzi wa hali ya juu na Maabara ya DNA ya Jiji la New York, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari na ofisi ya meya siku ya Ijumaa.

Ni mara ya kwanza kutambulia waathiriwa wa shambulizi dhidi ya Kituo cha Biashara cha Dunia tangu Septemba 2021. Hata hivyo, waathiriwa 1,104, sawa na asilimia 40 ya wale waliofariki, bado hawajatambuliwa, imesema taarifa hiyo.

Idadi ya watoa huduma ya kwanza ya kibinadamu wa matukio hayo ya 9/11 ambao wamekufa kutokana na matatizo ya afya waliyoyapata wakati wakiwa chini ya vifusi kuokoa watu ni karibu sawa na idadi ya watoa huduma hiyo waliokufa wakati wa mashambulizi.

"Wakati majengo yalipoanguka siku hiyo ya kutisha, tulipoteza Askari wa Zima Moto 343 wa Jiji la New York. ... Katika miaka yafuatayo, askari 341 wa FDNY (Idara ya Zima Moto ya New York) wamekufa kutokana na saratani na magonjwa adimu yaliyosababishwa na vumbi la sumu kwenye vifusi," Shirikisho la Askari wa Zima Moto la New York limeandika kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Facebook siku ya Jumatatu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha