

Lugha Nyingine
Mafuriko katika eneo la Libya Mashariki yaua zaidi ya watu 2,000
![]() |
Picha iliyopigwa Septemba 11, 2023 ikionyesha eneo lililoathiriwa na mafuriko huko Derna, Libya. (Serikali yenye makao yake mashariki mwa Libya/ Xinhua) |
TRIPOLI - Osama Hammad, Waziri Mkuu mwenye makao makuu yake Mashariki mwa Libya, amesema kuwa watu zaidi ya 2,000 wamefariki na watu wengine kwa maelfu hawajulikani walipo baada ya mafuriko kupiga Mashariki mwa Libya siku ya Jumapili.
Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini humo siku ya Jumatatu, Hammad amesema wengi wa waliopoteza maisha wameripotiwa katika mji wa bandari wa Derna, ambapo “eneo zima la makazi lilisombwa na mafuriko.”
Ametoa wito kwa wafanyakazi wa matibabu na timu za uokoaji nchini kote kutoa msaada kwa mji huo ulioathiriwa vibaya, wakati Naibu Waziri Mkuu wa Libya Mashariki Ali al-Gatrani ameomba msaada wa kimataifa kupitia chaneli ya TV ya Libya.
Mamlaka za eneo hilo zimetangaza siku tatu za maombolezo kwa watu waliofariki.
Kimbunga cha Bahari ya Mediterranean kilitua Mashariki mwa Libya siku ya Jumapili, na kusababisha mafuriko na kuharibu vifaa kwenye maeneo kilikopita.
Abdul-Hamed Dbeibah, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake makuu mjini Tripoli siku ya Jumapili aliagiza mamlaka husika kukaa katika hali ya tahadhari na kuchukua hatua za kukabiliana na kimbunga hicho, akiahidi "kuwalinda watu na kupunguza uharibifu."
Wizara ya Masuala ya Kijamii na Jumuiya ya Mwezi Mwekundu ya Libya imeanza kutoa msaada wa haraka kwa wale walioathiriwa na maafa.
Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta imekuwa na migawanyiko kwa miaka mingi kati ya tawala hasimu za mashariki na magharibi. Kila utawala unaungwa mkono na makundi yenye silaha na wanamgambo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma