"Kuendeleza tena Utandawazi kunaendana na maslahi yetu ya pamoja," asema Mwanauchumi Mwandamizi wa WTO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 14, 2023
Mwanauchumi Mwandamizi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ralph Ossa akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua kwenye makao makuu ya WTO huko Geneva, Uswisi, Septemba 12, 2023. (Xinhua/Lian Yi)

GENEVA - "Kuendeleza tena Utandawazi kunaendana na maslahi yetu ya pamoja," Ralph Ossa, Mwanauchumi Mwandamizi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi majuzi.

Kwa mujibu wa Ossa, kuendeleza tena utandawazi inamaanisha kuongezeka kwa ushirikiano wa kimataifa na muunganiko mpana wa kiuchumi ni muhimu katika kukabiliana na changamoto kubwa na kujenga mustakabali salama, jumuishi na endelevu.

Siku ya Jumanne, WTO ilichapisha toleo la Mwaka 2023 la Ripoti ya Biashara Duniani. Ripoti hii kinara inawasilisha ushahidi mpya wa manufaa ya ushirikiano wa kiuchumi ulio mpana na jumuishi zaidi, kwani dalili za mapema za mgawanyiko wa kibiashara zinatishia kupunguza ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Ripoti hiyo inalenga kufuta dhana ya kuongezeka kwa kauli za kutilia shaka biashara, ambazo zinadai kuwa biashara ya kimataifa ni kikwazo katika kujenga dunia salama, jumuishi na endelevu zaidi, amesema. Kauli kama hizo "ni tofauti kabisa na kauli ambayo imekuwa ikiongoza utungaji wa sera za biashara tangu Mwaka 1947."

"Utandawazi kwa kweli uko katika njia panda," wakati ambapo wimbi linakwenda kinyume nao, lakini bado kuna muda wa kuchukua hatua, amesema.

Mvutano wa sera za biashara unaongezeka na dalili za kwanza za mgawanyiko wa kiuchumi katika misingi ya siasa za kijiografia tayari zinaonekana, lakini biashara kwa ujumla imesimama imara, hivyo mazungumzo ya kuondoa utandawazi yametiwa chumvi, amebainisha.

"Gharama za kiuchumi kutokana na mgawanyiko zitakuwa kubwa," Ossa amesema. Mfano wa uhalisia ulioandaliwa na wanachumi wa WTO unaonesha kwamba katika mazingira ya hali mbaya zaidi ya ushindani kamili wa siasa za kijiografia, mapato ya kimataifa kwa wastani yatapungua kwa asilimia 5, na mtiririko wa biashara kwa wastani utapungua kwa asilimia 13, ameongeza.

Ili kudumisha amani na usalama, kupunguza umaskini na hali ya ukosefu wa usawa, na pia kufikia uchumi endelevu, "tunahitaji kukumbatia biashara na siyo kuikataa ... pia tunahitaji mfumo wa biashara wa pande nyingi," amesisitiza.

Akizungumzia nafasi ya China katika mchakato wa kuendeleza tena utandawazi, Ossa amesema kuwa China inaunga mkono mfumo wa biashara wa pande nyingi na pia utandawazi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha