Ndoto za vijana wa Zimbabwe zaruka juu kwenye anga ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 15, 2023
Ndoto za vijana wa Zimbabwe zaruka juu kwenye anga ya juu
Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding (wa nne kutoka kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Data za Kijiografia na Anga ya Juu la Zimbabwe (ZINGSA) Painos Gweme (wa tano kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Zimbabwe wa Shindano la Uchoraji la "Ndoto Yangu" mjini Harare, Zimbabwe, Septemba 13, 2023. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)

HARARE - Ubalozi wa China nchini Zimbabwe umefanya hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wawili wa Shindano la Uchoraji la "Ndoto Yangu" kwa vijana wa Afrika siku ya Jumatano.

Michoro kumi, ikiwa ni pamoja na ya msichana wa Zimbabwe Hope Mafiko, imeshinda Tuzo ya "Tian He", ambayo ni tuzo ya kwanza.

Akiwa ni mshindi wa tuzo ya kwanza, Mafiko amepokea tuzo yake katika ukumbi mkuu nchini China. Mchoro wake wenye maudhui ya "Mmoja wa Wasanifu Bora wa Maumbo ya Ndani barani Afrika," unaonyesha wasichana wawili wa Afrika wakitazama juu angani, ambayo inaonyesha kwa uwazi shauku ya binadamu kwa ulimwengu wa ajabu.

Asa King Zvihari mwenye umri wa miaka 24, mshindi mwingine, ameeleza kufurahia kuwa miongoni mwa washiriki bora zaidi barani Afrika. Zvihari ameshinda Tuzo ya "Meng Tian", tuzo ya tatu, kwa kazi yake yenye maudhui ya "Waafrika wote wameungana na kufanya kazi pamoja."

"Mchoro wangu unaonyesha nchi zote za Afrika zimeshikamana, zikifanya kazi pamoja kama nchi moja. Kwa hiyo katika Afrika hii iliyoungana, kuna faida zaidi. Kutakuwa na uwezeshaji. Kutakuwa na biashara huria kati ya nchi za Afrika, kutakuwa na ajira, na hakutakuwa na mipaka," Zvihari amesema. "Ninahisi kuhamasishwa, na ninahisi kuwa niko kwenye njia sahihi ya ustawishaji wa taaluma yangu. Natumai kuwa msanii anayetambulika kimataifa."

Shindano la "Ndoto Yangu" linalenga kuhimiza mabadilishano kati ya watu na ushirikiano katika masuala ya anga ya juu kati ya China na Afrika. Shindano la uchoraji limeandaliwa kwa pamoja na sekretarieti ya Kamati ya China ya utekelezaji wa matokeo ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), Ofisi ya Uhandisi wa Anga ya Juu ya China (CMSEO) na ujumbe wa China katika nchi za Afrika.

Siku ya Jumatano, wanaanga wa China walioko kwenye kituo cha anga ya juu cha China cha Tiangong walionyesha picha 10 za tuzo ya kwanza za vijana wa Afrika.

Washiriki wa Zimbabwe waliohudhuria hafla hiyo ya kukabidhi tuzo mjini Harare, Zimbabwe, pia walipata fursa ya kuungana na vijana wengine wa Afrika katika kipindi cha "zungumza na wanaanga" ambapo vijana wa Afrika walizungumza na wanaanga wa China walioko kwenye kituo cha anga ya juu cha China kwa njia ya video.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo, Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding amewapongeza vijana wa Zimbabwe kwa ushiriki wao na kutambuliwa kwao.

“Ninatumai kwa dhati kuwa shughuli ya leo itasaidia kupanda mbegu mpya za sayansi, sanaa, urafiki na ndoto akilini mwenu, ambapo naamini mbegu hizo zitaota mizizi, kustawi na kuzaa matunda,” Balozi Zhou amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha