Rais Xi Jinping na mwenzake Hichilema wa Zambia watangaza kuinua hadhi ya uhusiano kati ya China na Zambia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 18, 2023
Rais Xi Jinping na mwenzake Hichilema wa Zambia watangaza kuinua hadhi ya uhusiano kati ya China na Zambia
Rais Xi Jinping wa China na Mkewe Peng Liyuan wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na mkewe Mutinta Hichilema kabla ya mazungumzo kati ya Rais Xi na Hichilema mjini Beijing, China, Septemba 15, 2023. (Xinhua/Huang Jingwen)

Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo na mwenzake wa Zambia, Hakainde Hichilema, mjini Beijing ambapo wametangaza kuinua uhusiano kati ya China na Zambia kuwa wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote.

Kwenye mazungumzo hayo yaliyofanyika Ijumaa, Rais Xi amesema urafiki wa jadi ulioanzishwa na kizazi cha viongozi wakongwe wa nchi hizo mbili umestahimili majaribu ya mabadiliko ya mazingira ya kimataifa, na Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imekuwa alama ya urafiki kati ya China na Afrika.

Huku akisema China daima imekuwa ikitazama na kuendeleza uhusiano kati ya China na Zambia kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, Rais Xi amesema China inaiunga mkono Zambia katika kulinda mamlaka ya nchi, usalama na maslahi ya maendeleo ya taifa na kufuata njia ya maendeleo inayoendana na hali ya nchi yake. Rais Xi ameeleza nia ya China kuimarisha mawasiliano kati ya vyama na kubadilishana mawazo kuhusu uzoefu wa utawala wa nchi na Zambia.

Rais Xi huku akikaribisha bidhaa zaidi za Zambia kuingia katika soko la China amesema China inatarajia kujenga kwa pamoja Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na Zambia na kupanua ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu, kilimo, madini na nishati safi ili kufikia maendeleo na ustawi kwa pamoja.

Akieleza kuwa kujitokeza kwa pamoja kwa nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa ushawishi wao duniani kumekuwa mwelekeo usioweza kurudishwa nyuma wakati huu, Rais Xi amesema China na Zambia zinahitaji kuimarisha mshikamano na uratibu, kutekeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi na kushikilia kithabiti haki na usawa wa kimataifa.

Kwa upande wake Hichilema amesema Zambia inathamini urafiki ulioanzishwa na kizazi cha viongozi wakongwe wa nchi hizo mbili. Amesema, maendeleo ya China yamehimiza maendeleo ya nchi za Dunia ya Kusini, kuongeza uwakilishi na sauti zao katika masuala ya kimataifa, na kuhimiza maendeleo ya utaratibu wa kimataifa katika mwelekeo wa haki na halali zaidi.

Amesema, Zambia inaishukuru China kwa kuunga mkono Umoja wa Afrika kuingia katika Kundi la 20 (G20) na kufanya juhudi zaidi katika kushughulikia suala la deni la Zambia. Amesema nchi yake inafuata kanuni ya kuwepo kwa China moja, inathamini sana fikra na kanuni elekezi za maendeleo ya kisasa ya China, na inatumai kujifunza kutoka kwa uzoefu wa maendeleo wa China.

Hichilema amefanya ziara ya kiserikali nchini China kuanzia Septemba 10 hadi 16 kutokana na mwaliko wa Rais Xi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha