Mkutano wa kilele wa G77 na China wahitimishwa kwa msisitizo wa kuwezesha nchi za Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 18, 2023
Mkutano wa kilele wa G77 na China wahitimishwa kwa msisitizo wa kuwezesha nchi za Kusini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Mkutano wa Kilele wa Kundi la nchi 77 (G77) na China huko Havana, Cuba, Septemba 15, 2023. (Picha na Joaquin Hernandez/Xinhua)

HAVANA - Mkutano wa kilele wa siku mbili wa Kundi la nchi 77 (G77) na China umehitimishwa Jumamosi kwa kutoa wito kwa nchi za Kusini kushiriki na kutoa sauti zaidi katika mfumo wa usimamizi wa kimataifa.

Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka nchi zaidi ya 100, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 30.

Sauti yenye nguvu kwa Nchi za Kusini

Ukiangazia changamoto zinazokabili nchi za Kusini, mkutano huo umesisitiza haja ya utaratibu wa kimataifa ulio na usawa na umakini zaidi kwa nchi za Kusini.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa sauti ya Kundi la nchi 77 na China daima itakuwa muhimu kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Akitaja kundi hilo kama “mtetezi wa ushirikiano wa pande nyingi," Guterres ametoa wito kwa G77 na China "kutetea mfumo unaosimikwa katika usawa; kutetea mfumo ulio tayari kuondoa dhuluma na kupuuzwa kwa karne nyingi; na kutetea mfumo unaotoa huduma kwa binadamu wote na siyo kwa wenye haki maalumu."

Mchango wa China

Tangu miaka ya 1990, kwa kuhusika zaidi kwa China chini ya mfumo wa "G77 na China," kundi hilo limekuwa likibeba jukumu muhimu zaidi katika nyanja za kimataifa.

Katika hotuba yake ya ukaribisho kwenye mkutano huo, Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alisisitiza juhudi za China za kuhimiza ushirikiano wa kimataifa.

"Pendekezo la Maendeleo ya Dunia linalotolewa na Rais Xi Jinping wa China ni pendekezo jumuishi na thabiti katika kuweka utaratibu mpya wa kimataifa wenye haki na usawa," amesema.

Akitoa mfano wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja la China, Rais wa Visiwa vya Comoro na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Azali Assoumani amesema kwenye mkutano huo kuwa China inalenga kuweka mazingira yenye uwiano na jumuishi kwa kuzingatia ushirikiano watu wote.

Ikiwa ilianzishwa kwa mara ya kwanza Mwaka 1964, G77 sasa ina zaidi ya nchi wanachama 130, na uenyekiti wake unazunguka kati ya nchi wanachama wake wa Asia, Afrika, na Amerika Kusini kwa kuzingatia kanuni za kikanda.

China si mwanachama wa kundi hilo lakini imekuwa ikiunga mkono na kushirikiana na kundi hilo chini ya mfumo wa "G77 na China."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha