China yafanya shughuli ya kukumbuka vita dhidi ya uvamizi wa Japan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 19, 2023
China yafanya shughuli ya kukumbuka vita dhidi ya uvamizi wa Japan
Watu wakihudhuria hafla ya kukumbuka Tukio la Septemba 18 kwenye Jumba la Makumbusho ya Historia ya 9.18 huko Shenyang, Mji Mkuu wa Mkoa wa Liaoning, Kaskazini Mashariki mwa China, Septemba 18, 2023. (Picha na Chen Song/Xinhua)

SHENYANG - Wakati ving'ora vikilia huko Shenyang, Mji Mkuu wa Mkoa wa Liaoning, Kaskazini Mashariki mwa China siku ya Jumatatu, watembea kwa miguu walisimama kimya na magari yalipiga honi kukumbuka miaka 92 ya Tukio la Septemba 18 lililoashiria kuanza kwa uvamizi wa Japan dhidi ya nchi ya China.

Tangu Mwaka 1995, Mji wa Shenyang umekuwa ukipiga ving’ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga kila mwaka kwa kukumbuka Tukio la Septemba 18.

Hafla za kumbukumbu ya tukio hilo zimefanyika sehemu mbalimbali nchini China siku ya Jumatatu. Miji mingine mingi, ikiwa ni pamoja na Nanjing na Chengdu, pia ilipiga ving'ora siku hiyo ili kuwakumbusha watu kukumbuka historia na kuthamini amani.

Septemba 18, 1931, wanajeshi wa Japan walilipua sehemu ya reli iliyokuwa chini ya udhibiti wao karibu na Mji wa Shenyang na kushutumu wanajeshi wa China kuhusika na hujuma hiyo ili kutumia kama kisingizio cha mashambulizi yake. Baadaye usiku huo, walishambulia kambi karibu na Shenyang.

Juhudi za mapambano ya watu wa China baada ya Tukio la Septemba 18 ziliashiria mwanzo wa Vita vya mapambano ya Watu wa China dhidi ya Uvamizi wa Japan.

"Miaka 92 imepita, na sasa maisha yanazidi kuwa bora, lakini lazima tukumbuke daima kwamba lazima tuungane ili kujenga nchi yenye nguvu," Li Weibo, mwanajeshi mkongwe mwenye umri wa miaka 91 amesema.

Katika Jumba la Makumbusho ya Historia ya 9.18 huko Shenyang, watu wa hali mbalimbali walikusanyika na kufanya hafla ya kukumbuka Tukio la Septemba 18. Data za kumbukumbu za historia zinazoonyeshwa kwenye jumba hilo zinaelezea mpango wa muda mrefu wa jeshi la Japan wa kuivamia China.

"Kila mwaka karibu Septemba 18, Jumba la makumbusho hushuhudia ongezeko la utembeleaji, huku idadi ya watembeleaji kila siku ikikaribia 10,000. Watu huja kwa hiari kwenye jumba la makumbusho kukumbuka historia ya mateso, kukumbuka watu waliojitolea mhanga kwa imani, na kutambua moyo wao wa kitaifa," amesema Fan Lihong, mtunzaji wa jumba hilo la makumbusho.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha