Mapigano makali yaendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum huku pande zinazopigana zikishutumiana

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 19, 2023
Mapigano makali yaendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum huku pande zinazopigana zikishutumiana
Picha iliyopigwa Septemba 17, 2023 ikionyesha moto na moshi kutoka kwenye jengo huko Khartoum, Sudan. (Kundi la Mtandao wa WhatsApp la Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan/ Xinhua)

KHARTOUM - Mapigano makali yameendelea Jumatatu kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Askari wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), huku pande hizo mbili zikishutumiana kushambulia miundombinu muhimu katika mji mkuu, Khartoum.

SAF imeishutumu RSF kwa kuongoza kampeni ya kijeshi ya kuharibu mji mkuu, Khartoum.

"Wanamgambo wamechoma mioto dhidi ya taasisi kadhaa muhimu za kiuchumi na majengo ya kibiashara, ambayo ni nguzo za uchumi wa taifa," Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.

Wizara hiyo imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, serikali, na mashirika ya kimataifa, ya kikanda na ya haki za binadamu kulaani uhalifu wa RSF na kuianisha kuwa kundi la kigaidi.

Vipande vya video vilivyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili na Jumatatu, na kuthibitishwa na Shirika la Habari la China, Xinhua, vinaonyesha moto ukiteketeza majengo ya serikali na makao makuu Magharibi mwa Kamandi Mkuu wa Jeshi la Sudan katikati mwa Khartoum.

Moto huo umeteketeza jengo la Kampuni ya Uendeshaji ya Mafuta ya Greater Nile, mojawapo ya kampuni kubwa za mafuta nchini humo na pia kuteketeza jengo la Shirika la Viwango na Metrolojia la Sudan na jengo la Wizara ya Sheria ya Sudan.

Wakati huo huo, RSF imekanusha kushambulia makao makuu ya serikali na kuishutumu SAF kwa kufanya hivyo.

"Ndege za kivita za Jeshi la Sudan zimeendelea kushambulia kwa makusudi miundombinu na maeneo muhimu mjini Khartoum kwa lengo la kuyateketeza," RSF imesema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.

Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya SAF na RSF mjini Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15, na kusababisha vifo vya angalau watu 3,000 na wengine watu 6,000 kujeruhiwa, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Sudan.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha