

Lugha Nyingine
Rais wa Ghana ataka kulipwa fidia kwa biashara ya utumwa
UMOJA WA MATAIFA - Fidia lazima zilipwe kwa biashara ya utumwa ili kukabiliana na hali isiyo na usawa ya kihistoria ambayo inaathiri mfumo uliopo sasa wa Dunia, Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo amesema Jumatano.
“Ni wakati wa kukiri wazi kwamba sehemu kubwa ya Ulaya na Marekani zimejengwa kutokana na utajiri mkubwa uliovunwa na jasho, machozi, damu na vitisho vya biashara ya utumwa ya kupitia Bahari ya Atlantiki na unyonyaji wa karne nyingi wa wakoloni,” Rais Akufo-Addo ameuambia mjadala mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Haiwezi kuwa rahisi kujenga jamii zenye kujiamini na ustawi kutoka kwa nchi ambazo, kwa karne nyingi, maliasili zao ziliporwa na watu wao kuuzwa kama bidhaa, amebainisha.
"Hatutaki kukwepa jukumu lolote kwa matatizo yanayotukabili ambayo yametokana na sisi wenyewe, na inabidi kurudia kwamba hatutaki kuhurumiwa, na hatutaki kuwa kovu kwenye dhamiri ya mtu yeyote," Akufo-Addo amesema.
"Lakini, hatuwezi, na dunia haipaswi kujifanya kuwa hali ya sasa ya kiuchumi na kijamii ya Afrika haina uhusiano wowote na hali isiyo na usawa kihistoria ambayo imeunda mifumo ya sasa ya Dunia," ameongeza.
Ameeleza kuwa, kwa karne nyingi, Dunia haikuwa tayari na haikuweza kukabiliana na ukweli halisi wa matokeo ya biashara ya utumwa, lakini hatua kwa hatua hii inabadilika, na ni wakati wa kuleta mbele kwa uthabiti ajenda ya kulipa fidia.
"Fidia lazima zilipwe kwa biashara ya utumwa," Akufo-Addo amesema huku akipigiwa makofi mengi ya pongezi.
Pia ametaka fedha zilizoondoka kwa njia haramu kutoka Bara la Afrika kurejeshwa barani humo.
Wakati mustakabali wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu "siyo angavu sana," Rais Akufo-Addo ameelezea matumaini kwamba "tuna uwezo wa kubadilisha mambo."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma