Waghana zaidi wanufaika na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo unaofanywa na madaktari wa China (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 25, 2023
Waghana zaidi wanufaika na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo unaofanywa na madaktari wa China
Daktari wa China akimfanyia upasuaji mgonjwa wa mtoto wa jicho katika Hospitali ya LEKMA mjini Accra, Ghana, Septemba 20, 2023. (Picha na Seth/Xinhua)

ACCRA - Ni asubuhi mapema ya siku ya mwezi Septemba huko Accra, Ghana, ambapo watu wengi walikuwa wanajishughulisha na kazi zao za kila siku ili kujipatia riziki. Katika chumba cha upasuaji cha Hospitali ya LEKMA ya mji huo, inayojulikana kama Hospitali ya Urafiki wa China na Ghana, madaktari wawili wa macho wa China wanahudumia wagonjwa.

Katika asubuhi moja, madaktari hao wawili tayari wamefanya upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo kwa wagonjwa watatu ili kurejesha uwezo wao wa kuona, ambao ulikuwa umeharibika kutokana na ugonjwa wa macho.

Lei Peng, daktari mtaalamu wa macho kutoka Hospitali Kuu ya Pili ya Mkoa wa Guangdong, China ameungana na mwenzake Tang Xiaodi, daktari wa timu ya 12 ya madaktari wa China nchini Ghana, kufanya upasuaji wa bure wa mtoto wa jicho kwa wenyeji tangu Septemba 11.

Mpango huo wa wiki mbili wa kuwafikia wagongwa ni sehemu ya mradi wa upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo unaoitwa "Kuona Dunia Nzuri," ulioanzishwa na timu ya awamu iliyopita ya madaktari wa China Mwezi Novemba mwaka jana, kwa msaada kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wa China. Wawili hao wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba hadi kufikia Jumamosi, walikuwa wamekamilisha upasuaji 71, ambao umekaribia lengo la kufikia upasuaji 100.

Lei alikuwa mmoja wa timu ya madaktari wa China iliyofanya kazi nchini Ghana Mwaka 2016, na kutokana na mapenzi yake kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, aliamua kurejea kusaidia timu ya sasa katika kufanya upasuaji zaidi wa mtoto wa jicho bila malipo. “Upasuaji wa mtoto wa jicho huwapa mwanga watu, wakiwa walemavu wa macho kabisa wamekuwa mzigo kwa familia yao, lakini kama sasa wanaweza kuona, wanaweza kufanya kazi na kuiingizia kipato familia. Hiyo inaleta mabadiliko makubwa,” amesema.

Tangu Mwaka 2009, China imetuma timu 12 za madaktari nchini Ghana, zikijumuisha zaidi ya madaktari 100 ambao wametoa msaada muhimu kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Georgina Addy, 79, ni mmoja wa Waghana walionufaika na upasuaji wa bure wa kuondoa ugonjwa wa mtoto wa jicho alioupata miaka mitano iliyopita.

Addy ameliambia shirika la habari la China Xinhua baada ya kufanyiwa upasuaji kuwa alitafuta msaada katika hospitali nyingine kwa ajili ya tatizo lake la macho, lakini gharama kubwa ndiyo ilimzuia kufanyiwa upasuaji huo. “Jicho langu limekuwa likiuma sana, jirani yangu alipendekeza Hospitali ya LEKMA, nilikuja hapa Mwezi Agosti na kuripoti nikiwa na ripoti za maabara jana (Ijumaa), leo (Jumamosi) wametuleta kwenye chumba cha upasuaji, wakanifanyia upasuaji, na niko sawa sasa," amesema.

Mstaafu huyo ametoa shukrani zake kwa madaktari wa China ambao wameshughulikia mahitaji yake ya matibabu mara moja. "Nahisi kutuwa mzigo wangu wa kifedha. Wanasaidia Waghana, kwa hivyo tunawashukuru kwa dhati."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha