Msaada wa dharura wa China wawasili katika Nchi ya Libya iliyokumbwa na mafuriko (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 25, 2023
Msaada wa dharura wa China wawasili katika Nchi ya Libya iliyokumbwa na mafuriko
Ndege ya mizigo ya China iliyobeba misaada ya dharura ikiwasili katika Mji wa Benghazi, Mashariki mwa Libya, Septemba 24, 2023. (Picha na Ibrahim Hadia al-Majbri/Xinhua)

TRIPOLI - Ikiwa imebeba msaada wa dharura wa kibinadamu wenye uzito wa tani 90 kuelekea nchi ya Libya iliyokumbwa na mafuriko, ndege ya mizigo ya China imewasili Jumapili katika mji wa mashariki wa Libya, Benghazi.

Vifaa vya huduma ya kwanza, vifaa vya kusafisha maji, mahema, blanketi, mifumo ya uchunguzi wa ultrasound, jaketi za kujiokoa majini, na vifaa vingine vya msaada vimepakuliwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Benina, mbele ya Omar Abu-Dabous, Katibu Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Libya, pamoja na wanadiplomasia waandamizi wa Libya na China.

Septemba 10, Kimbunga Daniel cha Mediterranean, kilisababisha mafuriko mabaya zaidi nchini Libya katika miongo kadhaa iliyopita, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya eneo hilo, hasa miundombinu ya maji safi na maji taka.

Uchafuzi wa maji umesababisha watu kwa makumi kunywa sumu, haswa watoto, katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ambapo upatikanaji wa maji safi ni mdogo, kwa mujibu wa mamlaka ya Libya.

Akishuhudia makabidhiano hayo kwenye uwanja wa ndege, Kaimu Balozi wa China nchini Libya, Liu Jian, amesema kuna matumaini kuwa msaada wa China utasaidia Libya katika kukabiliana na athari za maafa na kurejesha katika hali ya kawaida maeneo yaliyoathirika.

Amesema China bado iko tayari kuwasiliana na kuratibu kwa pamoja na mamlaka ya Libya ili kutoa msaada zaidi kwa Libya katika operesheni yake ya uokoaji na utoaji misaada na kazi ya ujenzi mpya.

Pia katika uwanja wa ndege, Kaimu Balozi wa Libya nchini China Khaled Al-Sayah ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba msaada wa wakati uliotolewa na China unaonyesha urafiki mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

Hapo awali, Shirika la Msalaba Mwekundu la China lilikabidhi dola za Kimarekani 200,000 taslimu kwa Shirika la Hilali Nyekundu la Libya ikiwa ni msaada wa dharura wa kibinadamu kwa ajili ya juhudi za kukabiliana na majanga nchini humo baada ya kutokea kwa mafuriko hayo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha