AIIB yaidhinisha nchi wanachama wapya watatu katika mkutano wake wa kila mwaka nchini Misri (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 27, 2023
AIIB yaidhinisha nchi wanachama wapya watatu katika mkutano wake wa kila mwaka nchini Misri
Picha iliyopigwa Januari 13, 2021 ikionyesha jengo la makao makuu ya Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB) katika Mji wa Beijing, China. (Xinhua/Li Xin)

SHARM EL-SHEIKH - Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB) sasa ina nchi wanachama 109 baada ya Bodi ya Magavana wake kuidhinisha maombi ya El Salvador, Visiwa vya Solomon na Tanzania siku ya Jumanne.

Benki hiyo imeidhinisha maombi ya nchi hizo tatu kwenye mkutano wake wa nane wa mwaka uliofanyika Sharm El-Sheikh, Misri, AIIB imesema katika taarifa yake.

"AIIB ina rekodi ya mafanikio ya ushirikiano na wanachama wetu," Rais wa AIIB na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Jin Liqun amesema, huku akiongeza kuwa kushiriki kwa nchi hizo tatu "kutaimarisha jumuiya ya AIIB na kusaidia dhamira yetu ya pamoja ya kufadhili miundombinu kwa ajili ya kesho."

Nchi hizo tatu zitajiunga rasmi na AIIB mara tu zitakapokamilisha taratibu zinazohitajika na kuweka mtaji wa kwanza kwenye benki hiyo, imesema taarifa hiyo.

Nchi wanachama wa AIIB sasa kwa pamoja zinachukua asilimia 81 ya idadi ya watu wote duniani na asilimia 65 ya pato la taifa duniani, inasomeka taarifa hiyo.

AIIB ni benki ya maendeleo ya kimataifa ambayo dhamira yake ni kufadhili miundombinu ambayo inatoa kipaumbele katika uendelevu. Ilianza shughuli zake katika Mji wa Beijing, China Januari 2016.

Mkutano huo wa mwaka wa AIIB uliofanyika kwa siku mbili ulianza Jumatatu chini ya kaulimbiu isemayo "Ukuaji Endelevu wa Uchumi katika Dunia yenye Changamoto." 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha