

Lugha Nyingine
Ethiopia yaweka juhudi kuvutia watalii zaidi wa China (2)
![]() |
Picha ya kumbukumbu, iliyopigwa Juni 1, 2023, ikionyesha mandhari ya Bustani ya Urafiki huko Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Wang Ping) |
ADDIS ABABA - Juhudi zinaendelea kufanyika kuweka mazingira mazuri ya kuvutia watalii wa China ili kuingia katika soko kubwa la utalii la China, amesema Lelise Duga, Kamishna wa Kamisheni ya Utalii ya Jimbo la Oromia nchini Ethiopia.
"China ni soko kubwa la utalii. Tunataka kutumia vizuri hali hiyo kwa kujenga uwezo wetu, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wageni wa China kwa lugha yao na kufanya kazi kwa pamoja na serikali yao," Duga ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.
Amesema idadi ya watalii wa China wanaotembelea Jimbo la Oromia imeongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya serikali ya China kutangaza orodha ya nchi za kipaumbele kwa raia wake kutembelea barani Afrika na kwingineko.
Duga amesema watalii zaidi ya 20,000 wa China katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita wametembelea maeneo ya kitalii ya Oromia, jimbo kubwa zaidi katika taifa hilo la Afrika Mashariki, na karibu nusu ya watalii hao walikuwa wanaofanya kazi katika kampuni mbalimbali nchini Ethiopia.
"Soko jipya kwetu ni China na Mashariki ya Kati, ambazo raia wake wamezidi kupenda kusafiri sehemu mbali mbali za Dunia, haswa barani Afrika," Duga ameliambia Xinhua, huku akihusisha kuongezeka kwa watalii wa China katika eneo hilo na kuendelea kuongezeka kwa uchumi wa China na kiwango cha maisha ya raia wake.
Kamishna huyo amesema Kamisheni ya Utalii ya Oromia imeandaa waongoza watalii wenyeji ambao wanaweza kuzungumza Mandarin (lugha rasmi ya Kichina) na waendeshaji utalii wa China kama sehemu ya juhudi za kuvutia watalii zaidi kutoka China.
Kwa kutambua umuhimu wa soko la China kwa maendeleo ya utalii ya Ethiopia na kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya pande hizo mbili, kamisheni hiyo inashirikiana na kampuni za China kwa ajili ya ushirikiano wa kitamaduni na maendeleo ya lugha, ikilenga kuzalisha waongoza watalii watakaowasiliana kwa Lugha ya Kichina.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma