Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkakati wa siku za baadaye wakamilika huko Granada, Hispania (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 07, 2023
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkakati wa siku za baadaye wakamilika huko Granada, Hispania
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kilele usio rasmi wa Umoja wa Ulaya (EU) mjini Granada, Hispania, Oktoba 6, 2023. (Xinhua/Lian Yi)

GRANADA - Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) siku ya Ijumaa wamehitimisha mkutano wao wa kilele usio rasmi wa siku moja katika Mji wa Granada, Hispania ulioangazia mkakati wa siku za baadaye wa umoja huo na upanuzi wa nchi wanachama wapya kwa kupitishwa kwa tamko la Granada.

Viongozi hao walikusanyika katika mji huo wa kusini mwa Hispania ili "kuashiria mwanzo wa mchakato wa kufafanua mwelekeo wa jumla wa kisiasa na vipaumbele vya EU kwa miaka ijayo, kuweka mkakati wa kuchukua hatua kujenga mustakabali wetu wa pamoja kwa faida ya wote," linasomeka tamko hilo.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa kilele, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema kupitishwa kwa tamko hilo ni hatua muhimu ya kuanzia kwa kazi ya baadaye ya Ajenda ya Kimkakati ya EU (2024-2029). Mkutano huo wa Granada umekuwa ni wa mara ya kwanza kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kujadili vipaumbele vya siku za baadaye vya Ajenda, ambayo inatarajiwa kupitishwa Juni 2024.

Kuhusu upanuzi wa nchi wanachama wapya, tamko hilo limesema kuwa EU na nchi wanachama wa siku za baadaye zinahitaji kuwa tayari. "Nchi wanachama watarajiwa zinahitaji kuongeza juhudi zao za mageuzi ... Sambamba na hilo, EU inahitaji kuweka msingi wa kazi za kufanyika na mageuzi muhimu ya ndani."

"Mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya unazingatia sifa hitajika," Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, akiongeza kuwa "hakuna njia za mkato, hakuna kuingia kiotomatiki."

Upanuzi wa EU ni mchakato ambapo nchi hujiunga na kambi hiyo baada ya kutimiza seti ya masharti ya kisiasa na kiuchumi. Hivi sasa, nchi nane, zikiwemo kadhaa kutoka eneo la Balkan Magharibi, Ukraine na Moldova, zimepewa hadhi ya kuwa wanachama wanaowania kujiunga, lakini kila moja inafuata taratibu tofauti za kujiunga na EU.

Kaimu Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez, ambaye nchi yake kwa sasa inashikilia urais wa zamu wa miezi sita wa Baraza la Umoja wa Ulaya, alisema siku moja kabla ya mkutano huo kwamba Hispania daima iko wazi kwa upanuzi, lakini alibainisha kuwa kujumuisha nchi wanachama hawa wapya kutaleta "changamoto nyingi ndani ya EU."

Viongozi hao wa EU pia wamejadili sera ya uhamiaji. Hata hivyo, hakukuwa na kutajwa kwa suala la uhamiaji katika tamko la mkutano huo kutokana na mgawanyiko kati ya nchi wanachama.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha