

Lugha Nyingine
Timu za wachezaji wa China zapata medali 200 za dhahabu kwa rekodi bora zaidi katika Michezo ya Asia (4)
![]() |
Mchezaji wa China Zou Meirong (Kulia) akikwepa umakini wa mlinzi wa Korea Kusini wakati wa fainali ya mchezo wa magongo kwa wanawake. (Xinhua/Li An) |
HANGZHOU – Timu za wachezaji wa China zimejinyakulia medali 13 za dhahabu katika siku ya mwisho ya Michezo ya Asia ya Hangzhou, na kupata medali za dhahabu 200 kwa mara ya kwanza katika historia yake ya kushiriki kwenye Michezo ya Asia.
Tangu kufanyika kwa mara ya kwanza kwa michezo hiyo huko Tehran, Iran Mwaka 1974, rekodi bora zaidi ya hapo awali ya medali za dhahabu kwa timu za China ilitoka katika Michezo ya Asia ya Mwaka 2010 katika Mji wa Guangzhou, China wakati China ikiwa nchi mwenyeji iliposhinda medali za dhahabu 199.
Katika fainali ya Mchezo wa Xiangqi kwa wanaume iliyokutanisha wachezaji wote Wachina, mchezaji Zheng Weitong amemshinda mwenzake Zhao Xinxin na kutwaa medali ya 200 ya dhahabu kwa Timu mwenyeji ya China.
Mbio za kunyakua medali ya dhahabu za China zilianza katika mchezo wa mbio za kuogelea za marathon kwa wanaume, ambapo Zhang Ziyang aliibuka kidedea wakati wa asubuhi ya mvua.
Zhang alimaliza mbio hizo kwa kutumia saa 1:55:45.8, akifuatiwa kwa karibu na mchezaji mwingine wa China Lan Tianchen sekunde 0.4 tu nyuma. Park Jae-hun wa Korea Kusini alipata medali ya shaba.
China pia imeishinda Japan kwa seti 3-0 na kutetea taji la mchezo wa wavu kwa wanawake na kutwaa taji lake la tisa kwa jumla katika Michezo ya Asia.
Timu ya wachezaji wa China imemaliza mchezo wa magongo kwa wanawake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Korea Kusini na kushinda dhahabu. Ushindi huo pia umeipa China medali yake ya nne ya dhahabu katika Michezo ya Asia katika Mchezo wa Magongo kwa Wanawake na nafasi pekee ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto itakayofanyika Paris Mwaka 2024.
Korea Kusini imetwaa ubingwa wake wa tatu mfululizo wa soka kwa wanaume baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Japan katika mchezo wa fainali.
Ukiacha medali za dhahabu 200, timu za wachezaji wa China pia imepata medali 111 za fedha na 71 za shaba. Japan inafuatia ikiwa na medali za dhahabu 51, huku Korea Kusini ikishika nafasi ya tatu ikiwa na dhahabu 42.
Kabla ya sherehe za kufunga michezo hiyo leo Jumapili jioni, medali tatu za mwisho za dhahabu za Michezo ya Asia ya Hangzhou zitatolewa katika uogeleaji wa kisanaa na karate.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma