Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yafikia 232 (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 08, 2023
Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yafikia 232
Wapalestina wakipanda juu ya gari la kijeshi la Israeli katika Mji wa Gaza, Oktoba 7, 2023. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

GAZA - Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza imeongezeka hadi kufikia 232, huku wengine 1,697 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza siku ya Jumamosi. Wakati huo huo, idadi ya vifo miongoni mwa Waisraeli imevuka 200, na kufanya kuwa mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Israel katika miongo kadhaa iliyopita.

Mashambulizi hayo ya anga yametekelezwa kujibu mashambulizi ya awali ya roketi yaliyotekelezwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas) dhidi ya Israel.

Jeshi la Israel limethibitisha kwamba wanamgambo wa Kipalestina walikuwa wamerusha takriban roketi 3,000 dhidi ya Israel, na makumi ya wanamgambo hao walikuwa wamejipenyeza Kusini mwa Israel.

Hamas, kundi la wanamgambo linalodhibiti Ukanda wa Gaza, limedai kuwa limewakamata maafisa na wanajeshi kadhaa wa Israel, na kuongeza kuwa wanazuiliwa katika "maeneo salama."

Katika kujibu mashambulizi hayo, Jeshi la Israel limesema lililenga maeneo na makao makuu ya Hamas kwa kutumia makumi ya ndege za kivita katika maeneo mbalimbali ya pwani. Waziri wa Nishati wa Israel Israel Katz pia amesema nchi yake itakata usambazaji wa umeme katika eneo la Palestina kufuatia mashambulizi hayo ya Hamas.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza katika hotuba kwa taifa kwamba Israel ilikuwa "katika hali ya vita" na kuamuru "uhamasishaji na utayari wa askari wa akiba."

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amefanya mkutano wa dharura na maafisa waandamizi, akisisitiza haki ya watu wa Palestina kujilinda dhidi ya vikosi vya Israel na walowezi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha