Watalii kutoka China wawa muhimu kwa utalii wa Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 08, 2023
Watalii kutoka China wawa muhimu kwa utalii wa Misri
Watalii wa China wakitembelea Piramidi za Giza huko Giza, Misri, Oktoba 4, 2023. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO - Katika hekalu la Luxor, jumba kubwa la hekalu la kale la Misri lililoko ukingo wa mashariki wa Mto Nile, Huang Zhao, mtalii kutoka China, alikuwa akipiga picha huku akimsikiliza mwongoza watalii kuhusu historia ya hekalu hilo.

"Hekalu ni kazi bora ya sanaa. Nilikuwa nasoma vitabu vingi vya Historia ya Misri, na kutembelea maeneo hayo ya kiakiolojia ilikuwa ndoto," anasema Huang, ambaye pia alitembelea Piramidi Kuu zilizopo miji ya kusini mwa Misri ikiwa ni pamoja na Aswan, na maeneo ya kitalii ya baharini huko Hurghada.

Wakati huo huo, Chen Wu, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuja na wazazi wake kutoka Guangzhou, Mji Mkuu wa Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, anasema alikuwa amepanga safari hii ya Misri miaka miwili iliyopita.

"Baba yangu huwa ananihimiza kusoma vitabu vya historia, hasa kuhusu ustaarabu wa kale ambao unafanana na ule wa China," Chen anasema, huku akiongeza kuwa alikuwa akitunza pesa zake za matumizi kwa ajili ya kununua mifano ya kumbukumbu za kale kutoka katika masoko ya bidhaa za kale nchini Misri.

Kuimarika kwa sekta ya utalii nchini China sasa kunatoa msukumo mkubwa kwa utalii wa nje. Ongezeko hili la safari za nje limeenda sambamba na mojawapo ya likizo muhimu zaidi za kila mwaka za China, ambayo huitwa Wiki ya Dhahabu, iliyoanza Septemba 29 na kudumu kwa siku nane. Katika kipindi hiki, watu wa China wamesherehekea Sikukuu ya Taifa la China na Sikukuu ya Kijadi ya Mbalamwezi.

"Katika nchi hiyo ya uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, matumizi ya fedha kwa likizo na utalii wa ndani na nje yanatarajiwa kuongezeka, na hivyo kuchangia kuimarika kwa utalii duniani," amesema Mohamed Othman, Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko ya Utalii wa Utamaduni katika Misri ya Juu.

Kwa mujibu wa Taasisi Kuu ya Utalii ya China, taasisi ya utafiti yenye makao yake makuu mjini Beijing, maeneo ya nje ya China yalipokea wageni jumla ya milioni 40.37 kutoka China Bara katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

"Watalii wa China wameelimika sana na wana shauku kubwa ya kujifunza ustaarabu wa Misri na kusafiri kwa bajeti nzuri," mtaalamu huyo wa utalii amesema na kuongeza kuwa watalii wa China watasaidia kuimarisha sekta ya utalii ya Misri, ambayo ni moja ya vyanzo muhimu vya fedha za kigeni.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha