Israel yatangaza "hali ya vita" huku mapigano kati yake na Hamas yakiendelea (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 09, 2023
Israel yatangaza
Watu wakiwa wameshikilia miili ya watoto waliofariki katika shambulizi la anga la Israel kwenye Mji wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza Oktoba 8, 2023. (Picha na Khaled Omar/Xinhua)

JERUSALEM/GAZA - Baraza la mawaziri la Israel limetangaza "hali ya vita" siku ya Jumapili baada ya mashambulizi makubwa ya kushtukiza yaliyoanzishwa na Hamas ambayo hadi sasa yamewaua watu takriban 700 nchini Israel huku mashambulizi ya anga ya kulipiza kisasi ya Israel yakiua watu karibu 413 huko Gaza.

Jeshi la Israel limeendelea na mashambulizi yake makubwa ya anga katika maeneo lengwa ya Gaza siku ya Jumapili wakati ambapo wanamgambo wa Hamas wanaendelea kupigana na wanajeshi wa Israel katika maeneo ndani ya mipaka ya Israel.

Wanamgambo wa Hamas walikuwa wakiendelea kudhibiti jamii kadhaa za makazi Kusini mwa Israel Jumapili jioni, huku wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) wakipambana nao kwa risasi, Msemaji wa IDF Daniel Hagari amesema.

Zaka, shirika la uokoaji la Israel, limesema katika taarifa yake kwamba limekusanya miili ya wasichana na wanaume vijana takriban 260 waliokuwa wakiburudika katika tamasha la Nova, tukio la muziki la wazi katika eneo la mashambani karibu na uzio wa Gaza na Israel.

Watu wengi waliohudhuria tamasha hilo bado walikuwa hawajapatikana walipo hadi kufikia Jumapili usiku. Mitandao ya kijamii imefurika watu wakijaribu kutafuta jamaa na marafiki zao baada ya wanamgambo wa Hamas kuvamia tamasha hilo na maeneo mengine katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mashambulizi makubwa ya kushtukiza dhidi ya Israel yaliyohusisha kurusha maelfu ya roketi.

Ukatili zaidi

Kundi la wanamgambo wa Palestina Islamic Jihad (PIJ) ambalo linaendesha harakati zake katika ardhi za Palestina pia limejiunga na Hamas na kufanya mashambulizi dhidi ya Israel.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Jumapili, Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa PIJ, amesema kuwa kundi hilo linawashikilia Waisraeli 30 na kutangaza kwamba hawataachiliwa hadi pale wafungwa wa Kipalestina watakapoachiliwa kutoka jela za Israel.

Nje ya Gaza, wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon wanaoungwa mkono na Iran walishambuliana siku ya Jumapili kwa kufyatuliana makombora na roketi.

Katika jimbo la kaskazini la Misri la Alexandria, raia wawili wa Israel na mwongoza watalii wao mwenyeji wa Misri waliuawa walipokuwa kwenye ziara ya kundi la watalii wakati afisa wa usalama wa eneo hilo alipowafyatulia risasi.

Kwa kuonyesha uungaji mkono kwa Israel, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ametangaza Jumapili kuwa meli na ndege nyingi za kijeshi zitatumwa karibu na Israel.

Waisraeli walaumu kushindwa kwa ujasusi wa nchi

Tahariri katika gazeti la Ha'aretz la Israel iliyochapishwa siku ya Jumapili imekosoa vikosi vya usalama vya Israel kwa kile walichokiona kuwa ni "kushindwa kwa ujasusi na jeshi."

Tahariri hiyo pia imemlaumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa kuunda serikali ya mrengo mkali wa kulia ambayo ina mawaziri wanaounga mkono walowezi ambao walipuuza haki za Wapalestina na kuongeza hasira na kufadhaika za raia, mambo ambayo yamechangia katika mashambulizi ya hivi karibuni.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha