Israel yaimarisha nguvu za kijeshi kwenye mpaka na Gaza huku nchi za kikanda zenye nguvu zikihangaika kupata upatanishi (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 11, 2023
Israel yaimarisha nguvu za kijeshi kwenye mpaka na Gaza huku nchi za kikanda zenye nguvu zikihangaika kupata upatanishi
Watu wakitembea kuyapita majengo yaliyobomolewa kufuatia shambulizi la anga la Israel katika Mji wa Gaza, Oktoba 10, 2023. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

GAZA/JERUSALEM - Israel imezidisha mashambulizi yake ya anga siku ya Jumanne kwenye Ukanda wa Gaza na kuimarisha vikosi vyake mpakani, ikiwa ni siku ya nne katika moja ya mapigano makali zaidi kati ya Israel na kundi la Hamas kuwahi kutoka katika miongo kadhaa iliyopita.

Katika kulipiza kisasi, Hamas imerusha roketi mfululizo kulenga katikati ya Israel, ikiwa ni pamoja na Mji wa Tel Aviv.

Mgogoro huo umesababisha madhara makubwa kwa pande zote mbili. Wizara ya Afya ya Palestina imeripoti Jumanne kwamba idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya Israel huko Gaza imeongezeka hadi 900, na majeruhi 4,500. Wakati huo huo, watu takriban 1,008 wameuawa nchini Israel tangu Jumamosi, kwa mujibu wa televisheni ya habari ya Israel ya Kan.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameapa kulipiza kisasi kikubwa na kuidhinisha kurejesha askari akiba zaidi ya 60,000, na hivyo kufikisha jumla ya askari hao waliohamasishwa kufikia 360,000, ili kuweka mazingira kwa ajili ya mashambulizi ya ardhini yatakayowezekana kutokea.

Jeshi la Israel pia limewalenga maafisa wa Hamas, na kuwaua Waziri wa Uchumi wa Hamas, Jawad Abu Shamala na afisa mwingine mwandamizi, Zakaria Abu Muammar.

Huko Gaza, Israel inaendelea na mashambulizi yake makubwa ya anga na imesitisha usambazaji wa maji, umeme na chakula.

Mapema siku hiyo, mashambulizi ya anga ya Israel yalipiga kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Gaza na Misri, na kukatiza utoaji wa misaada ya kibinadamu. Mazungumzo kati ya Umoja wa Mataifa na maafisa wa Misri yanaendelea ili kuhakikisha msaada unaweza kupita katika kivuko hicho, huku Misri ikitafuta hakikisho kutoka Israel na Marekani.

Kama msuluhishi muhimu kati ya Israel na Palestina, Misri imekuwa ikiongeza juhudi za kumaliza mgogoro huo.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi ameonya Jumanne kwamba kujiimarisha kijeshi na mashambulizi yanayoendelea ni "hatari sana" na inaweza kuwa na athari kwa usalama na utulivu wa kikanda.

Amesisitiza dhamira ya Misri ya kupata suluhu ya kuunda nchi mbili na akahimiza mazungumzo ya amani ya haki na kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetangaza mkutano wa dharura utakaofanyika Jumatano. Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo watakutana kujadili mikakati inayolenga kupunguza mgogoro huo na kuzuia madhara zaidi kwa raia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha