Michezo ya Asia kwa Walemavu yafunguliwa rasmi katika Mji wa Hangzhou, China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 23, 2023
Michezo ya Asia kwa Walemavu yafunguliwa rasmi katika Mji wa Hangzhou, China
Mwogeleaji mlemavu wa China, Xu Jialing akiwasha moto wa mwenye wa michezo hiyo kwenye chombo maalum kwa mkono bandia wenye kutumia teknolojia za kisasa wakati wa hafla ya ufunguzi wa Michezo ya 4 ya Asia kwa Walemavu huko Hangzhou, Zhejiang, Mashariki mwa China, Oktoba 22, 2023. (Xinhua/Wu Zhizun)

HANGZHOU - Wiki mbili baada ya kufungwa kwa Michezo ya 19 ya Asia, Uwanja wa Olimpiki wa Hangzhou wenye umbo la ua la yungiyungi Mkoani Zhejiang, Mashariki mwa China umejawa tena na hali ya ushindani na ndoto za ushindi wakati Michezo ya 4 ya Asia kwa Walemavu ikifunguliwa Jumapili usiku.

Naibu Waziri Mkuu wa China Ding Xuexiang ametangaza kufunguliwa kwa Michezo ya Asia kwa Walemavu, wakati mashindano hayo yakirejea China kwa mara ya pili baada ya yale yaliyofanyika mara ya kwanza mjini Guangzhou mwaka 2010.

Chini ya kaulimbiu ya "Mioyo kukutana, Ndoto Kung’ara", hafla hiyo ya ufunguzi ilifikia kilele wakati mwogeleaji mlemavu wa China, Xu Jialing, aliyenyakua medali saba za dhahabu kwenye Michezo ya Asia kwa Walemavu ya Jakarta Mwaka 2018, alipowasha moto wa mwenge wa michezo hiyo kwenye chombo maalum kwa kutumia mkono bandia unaotumia teknolojia za kisasa, ikiwa ni msisitizo kwamba teknolojia inaweza kusaidia kutimiza ndoto.

Baada ya kuwashwa katika Mji wa Guangzhou, mwenge wa Michezo ya Asia kwa Walemavu ulifika kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Hangzhou baada ya kukimbizwa kwa siku tatu katika Mji wa Hangzhou, na mbio zake zilihitimishwa Jumamosi zikihusisha wakimbiza mwenge 600 wakiwemo watu 188 wenye ulemavu.

Wang Hao, Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya 4 ya Asia kwa Walemavu ya Hangzhou (HAPGOC) na Mkuu wa Mkoa wa Zhejiang, amewakaribisha washiriki wote na kuongeza kuwa lengo limekuwa ni kuandaa Michezo ya Asia na Michezo ya Asia kwa Walemavu ambayo ni ya kuvutia sana. Amesema,

"Mkoa wa Zhejiang unafanya juhudi ya kuwa eneo la kielelezo kwa ajili ya kufikia ustawi wa pamoja, ambapo kila mtu ana fursa ya kung’ara na kutimiza ndoto yake. "Mioyo kukutana, Ndoto Kung’ara" siyo tu kauli mbiu ya Michezo hii ya Asia kwa Walemavu, bali pia ni matarajio yetu ya pamoja."

Majid Rashed, Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Walemavu ya Asia (APC), ametoa shukrani zake kwa wanamichezo katika hotuba yake.

Takriban wanamichezo 3,100 kutoka nchi na maeneo 44 watashiriki katika vipengele 564 vinazohusisha michezo 22 kwenye Michezo hii itakayofanyika hadi Oktoba 28.

China imetangaza ujumbe wa washiriki 723 kwenye michezo hiyo, wakiwemo wanamichezo 439 watakaoshiriki kwenye vipengele 397 katika michezo 22.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha