China yatangaza wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-17 kwa ajili ya safari ya kwenda kituo cha anga ya juu (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 26, 2023
China yatangaza wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-17 kwa ajili ya safari ya kwenda kituo cha anga ya juu
Picha hii isiyo na tarehe ikionyesha wanaanga wa China Tang Hongbo (Kati), Tang Shengjie (Kulia) na Jiang Xinlin ambao watafanya safari ya anga ya juu kwenye Chombo cha Shenzhou-17. (Xinhua)

JIUQUAN - Wanaanga wa China Tang Hongbo, Tang Shengjie na Jiang Xinlin watafanya safari ya kwenda anga ya juu kwa kutumia Chombo cha Shenzhou-17, huku Tang Hongbo akiwa kamanda, Shirika la Anga ya Juu la China (CMSA) limetangaza Jumatano.

Ujumbe huo wa Chombo cha Shenzhou-17 una wanaanga wenye umri mdogo zaidi tangu kuanzishwa kwa ujenzi wa kituo cha anga ya juu cha China cha Tiangong. Pia ni timu ya kwanza ya wanaanga inayojumuisha mwanaanga mkongwe kutoka kundi la pili la wanaanga wa China na wanaanga wawili wachanga kutoka kundi la tatu la wanaanga.

Chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-17 kimepangwa kurushwa angani saa 5:14 asubuhi leo Alhamisi (Kwa saa za Beijing) kutoka Kituo cha Urushaji Satelaiti cha Jiuquan kilichoko Kaskazini Magharibi mwa China, Lin Xiqiang, Naibu Mkurugenzi wa CMSA, amesema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano.

Baada ya kujiunga na kundi la pili la wanaanga wa China Mwaka 2010, Tang Hongbo aliruka angani kwa mara ya kwanza katika safari ya miezi mitatu ya Chombo cha Shenzhou-12 Mwezi Juni, Mwaka 2021, ambao ulikuwa ni ujumbe wa kwanza wa wanaanga wa ujenzi wa kituo cha anga za juu cha China. Alipokea medali ya daraja la tatu na hadhi ya heshima ya "mwanaanga shujaa" Novemba 2021.

Akiwa kamanda wa ujumbe wa wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-17, Tang Hongbo atakuwa mwanaanga wa kwanza kurejea katika kituo cha anga ya juu cha China. Pia ameweka rekodi mpya ya muda mfupi zaidi kati ya safari mbili za anga ya juu kwa wanaanga wa China.

Tang Shengjie na Jiang Xinlin ni wapya kwenye safari ya anga ya juu. Walijiunga na kundi la tatu la wanaanga wa China Mwezi Septemba, Mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Lin, wanaanga hao wa Chombo cha Shenzhou-17 watafanya majaribio mbalimbali ya sayansi kwenye obiti ya anga ya juu na upimaji na majaribio ya matumizi ya upakiaji mzigo. Watafanya shughuli nje ya chombo cha anga ya juu(EVAs), kusakinisha mizigo ya ziada nje ya chombo cha anga ya juu na kufanya ukarabati wa kituo cha anga ya juu na kazi nyinginezo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha