

Lugha Nyingine
Uhusiano wa amani na wa ushirikiano kati ya China na Marekani ni muhimu kwa Dunia, asema Kissinger
NEW YORK - Uhusiano wa amani na wa ushirikiano kati ya China na Marekani ni muhimu kwa amani na maendeleo ya Dunia," Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Dkt. Henry A. Kissinger amesema Jumanne kwenye Tafrija ya Chakula cha Jioni ya kila mwaka ya Kamati ya Taifa ya Uhusiano kati ya Marekani na China (NCUSCR) mjini New York, Marekani.
"Nina imani nyote hapa mnakubali kwamba amani na maendeleo kati ya China na Marekani ni kwa ajili ya maslahi binafsi ya kila nchi na Dunia," amesema Dkt. Kissinger katika hotuba yake kwenye tafrija hiyo.
Wageni wote walioshiriki tafrija hiyo walipiga makofi wakiwa wamesimama ambayo ni maalum kwa kutimiza umri wa miaka mia moja wakati Kissinger alipowekwa jukwaani kwa kiti cha magurudumu. Na wengi wa wageni hao waliendelea kusimama hadi alipomaliza hotuba yake iliyochukua dakika zaidi ya 10.
"Nimetumia nusu ya maisha yangu kufanya kazi kwa ajili ya uhusiano kati ya Marekani na China ... napenda watu wa China, nimevutiwa na utamaduni wa China," amesema.
Dkt. Kissinger amesema ana hakika kwamba uhusiano kati ya China na Marekani unategemea "kuelewa kuwa nchi hizo mbili zina uwezo wa kipekee wa kuleta amani na maendeleo duniani, na pia zina uwezo wa kipekee wa kuharibu dunia ikiwa hazitashirikiana."
Ameelezea imani yake kuwa mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani yatapata njia za kuboresha uhusiano wao uliodorora. "Ninaamini sasa, kama nilivyoamini miaka 50 iliyopita, kwamba tunaweza kupata njia yetu kupitia matatizo haya."
Dkt. Kissinger ameonya kwamba Marekani inapaswa kushughulikia ipasavyo suala la Taiwan kwa kutilia maanani "Taarifa ya Shanghai," nyaraka ya kihistoria ambayo ilikuja kuwa msingi muhimu wa kisiasa kwa nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma