China yatoa wito wa ushirikiano wa usalama wa kimataifa katika Teknolojia za Akili Bandia (AI) (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 02, 2023
China yatoa wito wa ushirikiano wa usalama wa kimataifa katika Teknolojia za Akili Bandia (AI)
Picha iliyopigwa Septemba 22, 2022 ikionyesha kiwanda cha uzalishaji kwa kutumia teknolojia za akili bandia cha kampuni ya magari ya Great Wall (GWM) katika Wilaya ya Yongchuan Mjini Chongqing, Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Wang Quanchao)

BLETCHLEY PARK, UINGEREZA – Ujumbe wa China unaohudhuria Mkutano wa Usalama wa Teknolojia za Akili Bandia (AI) nchini Uingereza umetoa wito wa kuwepo ushirikiano na mabadilishano kati ya nchi mbalimbali kuhusu masuala ya usalama na usimamizi wa kimataifa wa teknolojia za akili bandia(AI).

Wu Zhaohui, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa China, amezungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha washiriki wote cha mkutano huo siku ya Jumatano, na ujumbe wa China umeshiriki katika majadiliano kuhusu usalama wa AI na masuala mengine.

Ujumbe wa China umepigia debe Pendekezo la Usimamizi wa AI Duniani lililotolewa kwenye Mkutano wa Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja uliofanyika mjini Beijing Oktoba 18, na utafanya mazungumzo ya pande mbili na nchi husika.

Ujumbe huo umesisitiza kwamba mkutano huo unatoa jukwaa muhimu la mazungumzo, na fursa za mabadilishano na ushirikiano kati ya nchi mbalimbali kuhusu usalama wa AI na masuala ya usimamizi wa kimataifa.

Ujumbe wa China umeshikilia kuwa usimamizi wa AI una mchango katika mustakabali wa binadamu wote, na ni jukumu la kushughulikiwa na nchi kote duniani.

Kwenye mkutano huo wa kilele, China imesisitiza kwamba, wakati zikiendeleza AI, nchi zinapaswa kutetea kwa dhati kanuni za kuwa na mwelekeo wa kuzingatia maslahi ya watu na kuendeleza AI kwa matumizi mazuri, kuimarisha usimamizi na udhibiti wa hatari za teknolojia, na kuhamasisha pande zote kushirikiana na kusimamia kwa pamoja kwa misingi ya kanuni za kuheshimiana, usawa na kunufaishana.

Ujumbe wa China umezitaka pande zote kuongeza uwakilishi wa nchi zinazoendelea katika usimamizi wa kimataifa wa AI, na kuziba pengo la teknolojia za akili bandia na uwezo wa usimamizi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha