

Lugha Nyingine
China yatuma msaada wa dharura kwa Nepal kwa ajili ya maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi (3)
POKHARA, Nepal – Shehena ya vifaa vya msaada wa dharura kutoka China kwa ajili ya maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi Magharibi mwa Nepal vimesafirishwa hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pokhara siku ya Jumatano ambapo ndege mbili za mizigo za China zilitua kwenye uwanja huo zikiwa na mahema 600 ya pamba na mablanketi 4,600 yenye thamani ya yuan milioni 5 (sawa na dola elfu 69 za Marekani).
Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nepal Narayan Kaji Shrestha na Balozi wa China nchini Nepal Chen Song walihudhuria hafla ya kukabidhi msaada huo.
Akihutubia kwenye hafla hiyo, Shrestha amebainisha kuwa China daima imekuwa ikiiunga mkono Nepal katika maendeleo yake ya kiuchumi, na kutoa msaada wakati Nepal ilipokumbwa na shida na inapohitaji msaada, kama vile wakati wa matetemeko ya ardhi ya Mwaka 2015 na janga la UVIKO-19.
"Tunafurahi kusema kwamba tuna marafiki kama China," amesema, huku akiongeza kuwa Nepal inasambaza vifaa hivyo vya msaada vya China katika wilaya za Jajarkot na Rukum Magharibi ambazo zilikumbwa na tetemeko la ardhi lenye nguvu ya richta ya 6.4 usiku wa Novemba 3.
Kwa upande wake Balozi Chen amesema vifaa hivyo vya misaada vinaonyesha kwamba China na Nepal zinaunganishwa na milima na mito na zina dhamana ya kusaidiana, pia vinaonyesha dhamira ya China ya kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu.
"Inajenga daraja la kuokoa maisha la mabadilishano kati ya watu chini ya Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na inaonyesha kikamilifu jinsi China inavyothamini ushirikiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Nepal unaojumuisha urafiki wa kudumu kwa maendeleo na ustawi," Chen ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma