

Lugha Nyingine
Israel yaapa kuzidisha mapigano Gaza licha ya kusimamisha vita kwa muda mfupi kila siku kwa ajili ya misaada ya kibinadamu (4)
![]() |
Moshi ukipaa angani kufuatia shambulizi la anga la Israel katika Mji wa Gaza, Novemba 9, 2023. (Xinhua) |
JERUSALEM - Israel imeapa siku ya Alhamisi kwamba vikosi vyake vitaendelea kuzidisha mapigano katikati ya Mji wa Gaza katika siku chache zijazo, licha ya kusimamisha vita kwa muda wa saa nne kila siku kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, ambapo Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) Herzi Halevi amezuru kaskazini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi akiwa na Ronen Bar, Mkuu wa Shirika la Usalama wa Ndani la Shin Bet akiwataka makamanda "kusonga mbele kwa nguvu, kwa utaratibu, na kuongeza kasi."
Viongozi hao wameonekana kwenye video zilizotolewa na jeshi wakiwa katika ziara yao huku wakiwa wameketi ndani ya kifaru kinachosonga mbele na baadaye kuzungumza na makamanda katika chumba chenye mwanga hafifu.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House ametangaza kuwa Israel imekubali kutekeleza usimamishaji vita kwa muda wa saa nne kila siku kuanzia Alhamisi kwa ajili ya misaada ya kibinadamu katika mashambulizi yake dhidi ya kaskazini mwa Gaza.
Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba usimamishaji huo wa vita ni katika maeneo maalum kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Amesisitiza kuwa hii haijumuishi usimamishaji wa mapigano na kwamba Israel "haitasimamisha mapigano kama bado kuna mateka huko Gaza na hatujafanikisha dhamira yetu: kuanguka kwa Hamas."
Katika mkutano tofauti na waandishi wa habari, Msemaji wa IDF Daniel Hagari amesema kuwa Jeshi la Israel lilianza siku ya Jumatano kutekeleza "usimamishaji vita wa ndani, wa kimbinu na wenye ukomo wa muda" katika mapigano ili kuwezesha raia kuhamia kusini. Ameongeza kuwa raia takriban 50,000 wamehamia kusini siku ya Alhamisi.
Wakati huo huo Vikosi vya Al-Quds, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina (PIJ) limetangaza katika taarifa yake kuwa liko tayari kuwaachia huru mateka wawili kwa sababu za kibinadamu.
Taarifa hiyo kwa Lugha ya Kiarabu imewataja mateka hao wawili kuwa ni "Hanna Katsir na mvulana Yagil Yaqoub," bila kutaja utaifa wao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma