Lugha Nyingine
Shenzhen, China mji wa teknolojia unaoeneza mitindo ya mapambo ya kuvaa duniani
Madini ya tanzanite kutoka Tanzania yakiwa ndani ya jumba la vito la Shenzhen. (People’s Daily Online) |
Mji wa Shenzhen katika Mkoa wa Guangdong, Kusini Mashariki mwa China unafahamika kuwa mji wa sayansi na teknolojia ya hali ya juu kama vile teknolojia za upashanaji habari na mawasiliano (TEHAMA) na teknolojia nyinginezo. Uvumbuzi mbalimbali katika mji huu umekuwa injini ya kuendelea kufuata sera ya China ya Mageuzi na Kufungua Mlango iliyoanza kutekelezwa miaka 45 iliyopita huku mji huu ukiwa ndiyo kinara mtangulizi.
Mji huu sasa si tu ni kituo cha teknoljia za TEHAMA na vifaa mbalimbali vya kidigitali, bali pia ni chimbuko la shughuli za mitindo, mavazi na uanamitindo ambapo bidhaa bora kama vile saa za mkononi na ukutani na vito na vidani vya kuvaa vimekuwa vikitoka katika mji huu na kuuzwa karibu duniani kote. Shenzhen, sasa ni mji wa mitindo.
Kwa mfano shughuli ya saa yenye historia ya miongo mingi ni moja ya shughuli za jadi hapa, pia ni nguvu muhimu katika shughuli ya kisasa ya mitindo ya Shenzhen. Eneo la Blight Time Valley ndilo hasa lenye shughuli nyingi za Saa. Kwa mujibu wa takwimu, kuna kampuni zaidi ya 1,500 za saa katika Mji wa Shenzhen, zenye kuzalisha mapato ya kila mwaka yenye thamani ya yuan bilioni 68. Uzalishaji wa saa wa hapa unachukua 53% ya uzalishaji wote wa China na 42% ya uzalishaji wote Duniani.
Aidha, sekta ya vito na vidani katika mji huu nayo imeendelea sana, ikiufanya mji huu kuwa hasa chimbuko la mitindo ya vidani inayoenea sehemu mbalimbali duniani. Eneo la Soko la Vito la Shuibei mjini Shenzhen ndilo hasa lenye pilika na shughuli nyingi husika likiwa na wafanyakazi zaidi ya 200,000 na thamani ya mauzo ya jumla ya kila mwaka ya karibu yuan bilioni 150.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma