Misri yapokea watoto njiti 28 kutoka hospitali kubwa zaidi ya Gaza (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 21, 2023
Misri yapokea watoto njiti 28 kutoka hospitali kubwa zaidi ya Gaza
Wahudumu wa afya wakimhamisha Mtoto njiti kutoka Ukanda wa Gaza katika upande wa Misri wa kivuko cha Rafah Novemba 20, 2023. (Kituo cha Habari cha Misri/Kutumwa Xinhua)

CAIRO - Misri imepokea watoto njiti 28 siku ya Jumatatu kutoka hospitali kubwa zaidi ya Gaza Al-Shifa, kupitia kivuko cha Rafah, kivuko pekee kinachounganisha Ukanda wa Gaza na Misri, imeripoti televisheni ya Misri ya AlQahera News.

Watoto 16 wamehamishiwa katika Hospitali Kuu ya El Arish katika Jimbo la Sinai Kaskazini, huku wengine wakielekea hospitali za Cairo, ripoti hiyo imeongeza.

Video za runinga zimeonyesha magari ya kubebea wagonjwa yakiwa na vifaa vya kukuza watoto yako tayari kwa ajili ya kutoa huduma muhimu ya dharura katika upande wa Misri wa Rafah.

Afya ya watoto hao wachanga inayozidi kuzorota haraka inawaweka katika hatari ya kufa mara moja, baada ya huduma za matibabu huko Al-Shifa kukatika.

Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Serikali ya Misri, nchi hiyo imepokea Wapalestina 236 waliojeruhiwa na watu 197 ambao ni wanafamilia wa watu hao waliojeruhiwa tangu Novemba 1.

Israel imekuwa ikifanya mashambulizi huko Gaza katika muda wa wiki kadhaa zilizopita kulipiza kisasi mashambulizi ya kushtukiza ya Kundi la Hamas katika eneo la Kusini mwa Israel yaliyotokea Oktoba 7, ambapo wanamgambo wa Hamas waliwaua takriban watu 1,200 na kuchukua mateka watu zaidi ya 200.

Ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Gaza ilitangaza Jumapili kwamba idadi ya vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza imezidi 13,000.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha