Kundi la Hamas laweka wazi undani wa mpango wake na Israel wa kusimamisha mapigano na mabadilishano ya wafungwa na mateka (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2023
Kundi la Hamas laweka wazi undani wa mpango wake na Israel wa kusimamisha mapigano na mabadilishano ya wafungwa na mateka
Watu wakifanya kazi ya uokoaji kwenye vifusi vya majengo yaliyobomolewa katika mashambulizi ya Israel kutoka angani dhidi ya mji wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Novemba 22, 2023. (Picha na Khaled Omar/Xinhua)

GAZA - Israel na Kundi la Vuguvugu la Upinzani wa Kiislamu la Gaza (Hamas) zimethibitisha Jumatano uwepo wa makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa siku nne katika Ukanda wa Gaza unaokumbwa na mgogoro, ili kuruhusu kupeleka misaada zaidi ya kibinadamu Gaza pamoja na mabadilishano ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Kundi hilo la kijeshi la Palestina na wapalestina waliofungwa kwenye jela nchini Israel.

Kusimamisha mapigano huko kwa ajili ya ubinadamu, ambako kumepatanishwa kwa juhudi za pamoja za Qatar, Misri na Marekani, kutawezesha kuachiliwa kwa mateka 50 wanaoshikiliwa Gaza, hasa watoto na wanawake na wengi wao ni raia wa nchi mbalimbali, kwa kubadilishana na Wapalestina takriban 150 wa kike na wa kiume waliofungwa jela nchini Israel, imesema Ikulu ya Israel na ofisa mkuu wa Hamas.

Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas Moussa Abu Marzouk ameliambia Shirika la Habari la Al Jazeera siku ya Jumatano kwamba usimamishaji vita huko Gaza utaanza saa 4:00 asubuhi kwa saa za huko (0800 GMT) leo Alhamisi.

Mateka hao wataachiliwa wachache wachache kwa muda wa siku nne, ambapo "kutakuwa na usimamishaji wa vita," imesema taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kuongeza kuwa kuachiliwa kwa kila mateka 10 zaidi kutasababisha kuongezwa kwa siku moja ya ziada katika kusimamisha vita.

Chanzo cha Kundi la Hamas kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba Hamas na Israel bado walikuwa wanakamilisha Jumatano usiku orodha yao ya mabadilishano ambayo ingekabidhiwa kwa kila upande.

Chini ya makubaliano hayo, malori zaidi ya misaada ya kibinadamu, dawa, na mafuta yataruhusiwa kuingia Gaza kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah ambacho kinaunganisha Gaza na Misri.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha