Qatar na Hamas zathibitisha kuongeza muda wa kusimamisha vita vya Gaza kwa siku mbili (7)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 28, 2023
Qatar na Hamas zathibitisha kuongeza muda wa kusimamisha vita vya Gaza kwa siku mbili
Watoto wakicheza kwenye uwanja wa michezo katika Mji wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Novemba 27, 2023. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

DOHA/GAZA - Qatar imetangaza Jumatatu kuwa Israel na Kundi la Hamas zimekubaliana kuongeza muda wa makubaliano ya sasa ya kusimamisha kwa muda mapigano kwa ajili ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza yaliyokuwa yafikie mwisho wake leo Jumanne kwa siku mbili zaidi.

Katika taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Qatar, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed Al Ansari amesema nchi yake inatumai "kusimamisha vita kwa muda kwa ajili ya kibinadamu kutasababisha usitishaji wa kudumu wa mapigano huko Gaza na kukomesha mauaji ya raia."

Taarifa hiyo ya kuongeza muda wa kusimamisha vita pia imethibitishwa na Kundi la Hamas. Kundi hilo limesema katika taarifa yake kwa Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba usimamishaji huo wa vita kwa muda utaongezwa kwa siku mbili zaidi "chini ya masharti yale yale yaliyoorodheshwa katika makubaliano ya awali."

Zikipatanishwa na Qatar, Misri na Marekani, Israel na Hamas zilifikia makubaliano ya kusimamisha vita kwa siku nne wiki iliyopita, ambayo yanahusu kusitisha uhasama huko Gaza, kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu katika eneo la Palestina, na kuachiliwa huru kwa mateka 50 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas kwa kubadilishana na wafungwa 150 wa Kipalestina kutoka jela za Israel.

Makubaliano hayo ya awali ya kusimamisha vita kwa muda huo yalianza kutekelezwa Ijumaa wiki iliyopita na yanatazamiwa kumalizika leo Jumanne.

Tangu mgogoro kati ya Israel na Hamas ulipozuka Oktoba 7, Qatar imekuwa ikifanya juhudi za upatanishi pamoja na Misri na Marekani kati ya pande hizo mbili zinazopigana ili kufanikisha kuachiliwa huru kwa mateka na kupunguza hali chochezi katika eneo hilo la Palestina.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha