

Lugha Nyingine
Idadi ya vifo vya Wapalestina yaongezeka hadi 15,899 mjini Gaza
![]() |
Watu wakikagua uharibifu baada ya mashambulizi ya Israeli katika Mji wa Rafah ulioko Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Desemba 4, 2023. (Picha na Khaled Omar/Xinhua) |
GAZA - Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 imeongezeka hadi 15,899, Ashraf al-Qedra, Msemaji wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na Kundi la Hamas amesema siku ya Jumatatu kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Khan Yunis, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, huku pia akisema kuwa idadi ya watu waliojeruhiwa imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 42,000, ambapo asilimia 70 ya waathirika ni watoto na wanawake.
Al-Qedra ameishutumu Israel kwa kuzidisha mashambulizi yake yanayolenga hospitali na vituo vya afya, akibainisha kuwa, imebomoa taasisi 56 za afya, kukamata wahudumu wa afya 35, na kuufanya mfumo wa afya katika Ukanda wa Gaza kushindwa kufanya kazi.
Al-Qedra ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani kulinda hospitali na timu za afya na za kibinadamu na kutoa njia salama kwa ajili ya vifaa tiba na mafuta kuingia Gaza na majeruhi kuondoa kutoka Gaza.
Wakati huo huo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), limesema Kundi la Hamas limejipenyeza kimakusudi miongoni mwa raia ili watu wa Gaza waweze kubeba madhara ya "ukatili wa Hamas."
"Vita vyetu ni dhidi ya Hamas, siyo watu wa Gaza. Tunachukua hatua za pande zote kupunguza madhara kwa raia ambao Hamas inawatumia kama ngao," IDF imesema katika taarifa yake kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X siku ya Jumatatu jioni.
Tangu Oktoba 7, Israel imekuwa ikiendesha vita vikubwa dhidi ya Kundi la Hamas baada ya wanamgambo hao kuanzisha mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo awali katika miji ya Israel.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma