Wiki ya mitindo ya Afrika yafunguliwa nchini Kenya kuonyesha mavazi ya kiasili

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 05, 2023
Wiki ya mitindo ya Afrika yafunguliwa nchini Kenya kuonyesha mavazi ya kiasili
Wabunifu wakitengeneza nguo kwenye Wiki ya Mitindo ya Afrika jijini Nairobi, Kenya, Desemba 4, 2023. (Xinhua/Han Xu)

NAIROBI – Awamu ya Pili ya Wiki ya Mitindo ya Afrika inayofanyika kuanzia Desemba 4 hadi 9 ikichanganya mitindo, tamaduni na ubunifu na ikilenga kuongeza kuonekana kwa aina nyingi za mavazi ya bara hilo imefunguliwa jijini Nairobi, Kenya siku ya Jumatatu, huku wabunifu kutoka nchi mbalimbali barani humo wakionyesha mavazi ya kiasili.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wiki ya Mitindo ya Afrika, Saitoti Meitamei, amesema lengo lake kuu ni kuendeleza vipaji vya ubunifu, ujasiriamali, uvumbuzi na kupanua soko la nguo za asili.

"Wiki ya Mitindo ya Afrika inahusu kurudisha fahari yetu, kuhakikisha kwamba Waafrika wanajivunia nguo ambazo zimetengenezwa Afrika," Meitamei amesema, huku akiongeza kuwa kampuni za kibiashara zimeunga mkono wiki hiyo ya mitindo.

Wabunifu zaidi ya 30 wa mitindo ya nguo wa Afrika wanaonyesha kazi zao kwenye shughuli hiyo huku wanamitindo zaidi ya 60 wakionyesha mavazi yaliyotengenezwa barani humo, Meitamei amesema, akiongeza kuwa wanafunzi wa ubunifu wa mavazi katika Chuo cha Ufundi cha Delight chenye makao yake makuu Nairobi, ambao ni waandaaji wa Wiki ya Mitindo ya Afrika, pia watashiriki kuonyesha mavazi yao kwa wanunuzi watarajiwa.

Meitamei amesema wabunifu watakaoonyesha mavazi yao ya asili katika wiki hiyo ya mitindo itakayofanyika chini ya kaulimbiu ya "usherehekeaji wa tamaduni, ubunifu na rangi" wamealikwa kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Ethiopia, Rwanda, Burundi na Kenya.

Wairimu Wangu, mratibu wa shughuli hiyo ya Wiki ya Mitindo ya Afrika, amesema mavazi ya asilia ya Afrika yameendelezwa, na kutoa njia endelevu za mapato kwa wabunifu vijana.

Kwa mujibu wa Wangu, kuandaliwa kwa Wiki ya Mitindo ya Afrika mwaka huu kumetokana na haja ya kujenga jukwaa kwa wabunifu kuonyesha bidhaa zao, na kuunganishwa na wateja wa ndani na nje ya Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha