Reli ya China-Laos yaongeza shughuli za utalii na ajira kwa wenyeji

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2023
Reli ya China-Laos yaongeza shughuli za utalii na ajira kwa wenyeji
Abiria wakiwa kwenye foleni katika Stesheni ya Reli ya Luang Prabang ya Reli ya China-Laos mjini Luang Prabang, Laos, Desemba 4, 2023. (Xinhua/Lu Yun)

VIENTIANE - Katika umri wa miaka 20, msichana wa Laos Bounmee tayari alikuwa mkimu wa familia yake. Akiwa mhudumu mkuu wa treni ya mwendokasi ya Reli ya China-Laos, sasa anapata mshahara mkubwa zaidi kuliko wenzake. Katika miaka miwili iliyopita tangu ianze kufanya kazi, reli hiyo imetoa fursa za ajira kwa maelfu ya watu wa Laos kama Bounmee, na kuleta faida halisi kwa utalii wa ndani, kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo baada ya janga la UVIKO-19.

"Wazazi wangu wananionea fahari sana," amesema kwa Lugha ya Kichina fasaha. Baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari ya juu, alienda kusoma Lugha ya Kichina kwa matumaini kwamba ujuzi wa lugha hiyo ungeweza kumsaidia kupata kazi yenye malipo makubwa, na kuzinduliwa kwa Reli ya China-Laos Desemba 3, 2021 kumesaidia juhudi zake kuleta matunda.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, reli hiyo imeshughulikia safari za abiria milioni 24.2 na kusafirisha mizigo yenye uzito wa tani milioni 29.1, kwa mujibu wa shirika la uendeshaji wa reli hiyo la China. Safari za kila mwezi za abiria katika reli hiyo zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka zaidi ya 600,000 mwanzoni mwa uzinduzi wake hadi zaidi ya milioni 1.1 kwa sasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Reli la Laos-China (LCRC), ambalo ni shirika la ubia lenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Laos, Vientiane linalohusika na uendeshaji wa sehemu ya Laos ya reli hiyo, mahitaji ya safari za treni za mwendokasi ni zaidi ya matarajio ya awali, na shirika hilo linafanya juhudi kuendana na mahitaji ya watu wa Laos yanayozidi kuongezeka na kuwa ya aina mbalimbali kila mara.

"Tunataka kuleta bidhaa na huduma bora kwa Laos, na tunataka watu wa Laos wanufaika," meneja wa uendeshaji wa LCRC amesema.

Reli hiyo imetoa mchango mkubwa katika ufufukaji wa tasnia ya utalii nchini Laos, ambayo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi lakini iliathiriwa vibaya na janga la UVIKO-19. Reli ya mwendokasi imekuwa kichocheo cha kiuchumi kinachohitajika sana, kwani imepunguza sana muda wa kusafiri kati ya miji mikubwa, kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Katika eneo la Luang Prabang, kivutio maarufu cha watalii, abiria walikuwa wakipanga foleni kuchukua treni za mwendokasi. Kutokana na Reli hiyo ya China-Laos, muda wa kusafiri kati ya Vientiane na Luang Prabang umepunguzwa hadi takriban saa 2, ikilinganishwa na saa zaidi ya 6 za kuendesha gari.

"Tumechagua Laos kama eneo la kutalii kwa sababu ni rahisi kusafiri kupitia treni," amesema Minjung Choi, mtalii kutoka Korea Kusini, ambaye alikuwa katika safari ya siku tano nchini Laos na rafiki yake.

Zaidi ya watalii milioni 2.4 wa kigeni walitembelea Laos katika miezi tisa ya kwanza ya 2023, ikiwa ni ongezeko la hadi asilimia 285 kutoka mwaka mmoja uliopita, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii ya Laos.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha