Israel na Kundi la Hamas wapigana vikali mjini Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 07, 2023
Israel na Kundi la Hamas wapigana vikali mjini Gaza
Picha hii iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Desemba 3, 2023 ikionyesha wanajeshi wa Israel wakiendesha operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza. (Xinhua)

GAZA - Wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Kundi la Hamas wamepigana katika vita vikali vya ana kwa ana kwa ajili ya kuudhibiti Mji wa Khan Younis, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa wa Gaza, huku kukiwa na mapigano makali katika ukanda huo, na kuzuia usambazaji wa misaada inayohitajika ambapo Jeshi la Israel limesema katika taarifa yake kwamba makomando wa Israel wamefika "kwenye kiini cha Mji wa Khan Younis" na kuuzingira.

Jeshi hilo limesema, vikosi vya ardhini na anga vimeanzisha mashambulizi katika mji huo, na kuua wanamgambo "kadhaa", na kubomoa mahandaki takriban 30, na kuvamia kituo cha Jeshi cha Hamas, ambapo silaha zimekamatwa na kuharibiwa.

Wakati huohuo wanajeshi wa Israel wameendelea na mashambulizi yao Kaskazini mwa Gaza huku "mapigano makali" yakiendelea hasa katika miji ya Jabalia na Shujaiya. Maeneo zaidi ya 250 yameshambuliwa katika siku iliyopita.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema katika hotuba yake kwa njia ya video kwamba vikosi vya Israel "vinazingira" nyumba ya Yahya Sinwar, Kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza. "Nyumba yake sio ngome yake, na anaweza kukimbia, lakini ni suala la muda hadi tutakapompata," Netanyahu amesema.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Daniel Hagari amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba Sinwar hayupo nyumbani kwake. "Yuko chini ya ardhi," Hagari amesema. "Sitaki kusema yuko wapi na vipi tunaweza kumpata na ni taarifa gani za kipelelezi tunazo (juu ya mahali alipo)," Hagari amesema.

Hagari amethibitisha kwamba moja ya malengo ya mashambulizi hayo, yaliyosababishwa na mashambulizi mabaya ya Hamasi Oktoba 7 Kusini mwa Israeli, ni "kumkamata Sinwar na kumuua."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, katika muda wa siku tatu zilizopita, usambazaji wa maji na unga umewezekana katika eneo la Rafah tu kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya barabara katika eneo hilo.

Watu takriban milioni 1.87 wa Gaza wamelazimika kuyakimbia makazi yao tangu kuanza kwa mgogoro huo, umesema Umoja wa Mataifa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha