

Lugha Nyingine
Kiongozi wa Hamas asema yuko tayari kujadiliana na Israel kuhusu kusimamisha mapigano Gaza
![]() |
Watoto wa Palestina wakionekana kwenye makazi ya muda katika Mji wa wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Desemba 13, 2023 (Picha na Yasser Qudih/Xinhua) |
GAZA - Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh amesema Jumatano katika hotuba yake kwa njia ya televisheni iliyorushwa kwenye kituo cha televisheni cha Al-Aqsa chenye uhusiano na Hamas kwamba kundi hilo la Palestina linalotawala Gaza liko tayari kujadiliana na Israel mpango au pendekezo lolote ambalo linaweza kufikia usimamishaji wa vita katika Ukanda wa Gaza huku akiongeza kuwa, mpango wowote kuhusu mustakabali wa Gaza bila Hamas hautafanikiwa.
"Tuko wazi kujadili mpango au pendekezo lolote ambalo linaweza kumaliza uvamizi (wa Israeli)," Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas, amesema.
Haniyeh amesema Hamas imekaribisha azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kutaka kusimamishwa mara moja kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza, na kupongeza juhudi za Saudi Arabia na kamati ya mawaziri iliyoundwa na Mkutano wa Maalum wa Pamoja wa Jumuiya za Nchi za Kiarabu na Kiislamu ili kumaliza mgogoro wa Gaza.
Amethibitisha kukataa kwa Hamas mipango yoyote ya kisiasa ya baada ya vita ambayo haijumuishi Kundi la Hamas na mirengo mingine ya Palestina, na akahimiza jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo ili kusitisha mashambulizi ya Israel mjini Gaza.
Hapo awali, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuondoka kwa viongozi kadhaa wa Hamas kutoka Qatar hadi maeneo yasiyojulikana, vikidai uwezekano wa viongozi hao kuhamia hadi nchi kama vile Lebanon, Iran, au Algeria.
Hakuna uthibitisho wowote kutoka kwa Hamas uliopatikana kuhusu ripoti hizi.
Mapigano kati ya Israel na Hamas tangu Oktoba 7 yamesababisha hasara kubwa. Wapalestina takriban 18,608 wameuawa na wengine 50,594 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na watu takriban 1,200 wamefariki katika mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma