Serikali ya mpito ya Guinea yatangaza hatua za usalama huku moto kwenye ghala ya mafuta ukiendelea katika mji mkuu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 19, 2023
Serikali ya mpito ya Guinea yatangaza hatua za usalama huku moto kwenye ghala ya mafuta ukiendelea katika mji mkuu
Picha hii iliyopigwa Desemba 18, 2023 ikionyesha moto baada ya mlipuko kwenye ghala la mafuta mjini Conakry, Guinea. (Xinhua)

CONAKRY - Serikali ya mpito ya Guinea Jumatatu imewataka wafanyakazi wote wasio wa lazima kubaki majumbani huku moto mkubwa uliozuka Jumapili usiku kwenye ghala kubwa la mafuta katika Eneo la Kaloum lililo katika Mji Mkuu wa Guinea, Conakry, ukiwa bado unaendelea kupamba moto.

"Wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi, isipokuwa vikosi vya ulinzi na usalama na sekta za matibabu, wanatakiwa kubaki nyumbani. Shule za umma na za kibinafsi zitafungwa na vituo vya huduma vitafungwa, isipokuwa huduma za afya," serikali ya mpito imetangaza katika taarifa kwa vyombo vya habari ambayo Shirika la Habari la China, Xinhua limepata nakala yake, ikielezea hatua za kwanza za usalama ambazo zimechukuliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chanzo cha moto huo katika ghala kuu la mafuta la Kampuni ya Petroli ya Guinean katika Eneo la Kaloum, ambalo ni eneo la utawala na biashara katika mji mkuu, bado hakijajulikana.

"Tunawaomba wakazi wa maeneo ya jirani kukaa mbali kutoka kwenye eneo siyo tu kwa ajili ya usalama wao wenyewe bali pia kuruhusu huduma kufanya kazi kwa usalama kamili," serikali imeeleza katika taarifa hiyo.

Mara tu baada ya moto huo kuzuka, vitengo vyote maalum vilishiriki mara moja na kuendelea kuuzima moto huo. Rasilimali za ziada zinatumwa kudhibiti moto huo na kupunguza athari zake.

Hakuna idadi rasmi kutoka serikalini ya watu waliofariki au kupata madhara hadi sasa, lakini mashuhuda wamemwambia mwandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka Kaloum kuwa watu zaidi ya kumi wamefariki dunia na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa vibaya. Aidha, uharibifu mkubwa wa mali umeshuhudiwa huku kukiwa na majengo, ofisi na magari yaliyoungua moto.

Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha