

Lugha Nyingine
China yaongeza kasi ya kutoa msaada kwa mikoa iliyokumbwa na tetemeko la ardhi (2)
Beijing - Serikali ya China inaongeza kasi ya kutoa msaada katika Mikoa ya Gansu na Qinghai Kaskazini Magharibi mwa China baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.2 lililotokea usiku wa manane siku ya Jumatatu kuua watu zaidi ya 100 ambapo Wizara ya Fedha na Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China siku ya Jumanne zimetenga Yuan milioni 200 (takriban dola za Kimarekani Milioni 28.18) kwa ajili ya mikoa hiyo. Kati ya fedha hizo, yuan milioni 150 zitatumika kusaidia Mkoa wa Gansu, wakati yuan milioni 50 zitaenda Mkoa wa Qinghai.
Shehena ya pili ya bidhaa za msaada, ikiwa ni pamoja na mahema 2,500 ya pamba, makoti ya baridi 20,000 na vitanda 5,000, vimetumwa Gansu, na Mkoa wa Qinghai pia umepokea mahema 1,500, makoti 5,000 ya pamba na vitanda 5,000, miongoni mwa vifaa vingine vya msaada. Hadi kufikia Jumanne asubuhi, vitu jumla ya 111,500 vya msaada vimetengwa kwa serikali za mitaa kusaidia mahitaji ya kimsingi ya watu walioathiriwa.
Tetemeko hilo lilitokea saa 5:59 usiku siku ya Jumatatu na lilikuwa na kina cha kilomita 10. Eneo lililoathirika zaidi la Mji wa Liugou liko umbali wa kilomita takriban 8 kutoka Wilaya inayojiendesha ya Makabila ya Wabao'an, Wadongxiang, Wasalar ya Jishishan katika Eneo linalojiendesha la Kabila la Wahui la Linxia, Mkoa wa Gansu.
Katika mkoa huo wa Gansu pekee, idadi ya vifo kutokana na tetemeko hilo la ardhi imeongezeka hadi 105, kwa mujibu wa serikali za mitaa. Tetemeko hilo pia limesababisha vifo vya watu 13 katika mkoa jirani wa Qinghai.
Wizara ya Uchukuzi ya China imesema, mtandao wa barabara karibu na eneo hilo lililoathirika zaidi unafanya kazi kawaida. Katika sehemu ambazo hali ya kuharibiwa kwa barabara na miundo ya madaraja imeripotiwa, upitaji wa magari na vyombo vya usafiri umerejeshwa kufuatia kazi ya awali ya ukarabati.
Usafirishaji wa umeme katika eneo la Jishishan umeanza tena kwa kiasi kikubwa. Shirika la Gridi ya Taifa la China limesema, umeme umerejeshwa kwa asilimia 88.36 ya watumiaji, na mashine za kuzalisha umeme za kituo cha karibu cha umeme cha Liujiaxia zinafanya kazi kawaida.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma