Rais Xi Jinping wa China akutana na Waziri Mkuu wa Russia, Mikhail Mishustin

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 21, 2023
Rais Xi Jinping wa China akutana na Waziri Mkuu wa Russia, Mikhail Mishustin
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin mjini Beijing, China, Desemba 20, 2023. (Xinhua/Huang Jingwen)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amekutana na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin mjini Beijing siku ya Jumatano akisema kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu, amekutana na Rais Putin mara mbili na kwamba serikali, mabunge, vyama vya siasa na serikali za mitaa za nchi hizo mbili zimefanya mawasiliano ya kina, na ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali umestawi kwa njia nzuri na thabiti.

Amesema, katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka huu, biashara kati ya China na Russia ilifikia lengo la biashara la thamani ya dola bilioni 200 kwa mwaka lililowekwa kwa pamoja na wakuu wa nchi hizo mbili, hali ambayo inaonyesha uhimilivu mkubwa na matarajio mapana ya ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili.

Ameeleza kuwa, kudumisha na kuendeleza uhusiano kati ya China na Russia ni chaguo la kimkakati lililofanywa na pande zote mbili kwa kuzingatia maslahi ya kimsingi ya watu wa pande zote mbili.

China inaunga mkono watu wa Russia kufuata njia ya maendeleo iliyochaguliwa na wao wenyewe, Rais Xi amesema, huku akielezea matumaini yake ya kuchukua maadhimisho ya kutimia miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Russia mwaka ujao kama mwanzo mpya ili kuendelea kupanua matokeo chanya ya uhusiano wa ngazi ya juu wa kisiasa na kusonga mbele kwa pamoja katika mchakato wa kuhamasisha kikamilifu maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kufikia ustawishaji wa mataifa hayo mawili.

Rais Xi ametoa wito kwa pande hizo mbili kutoa mchango kamili kwa manufaa ya kuaminiana kisiasa, kuendana kiuchumi, muunganisho wa miundombinu na mabadilishano kati ya watu; kuendelea kupanua ushirikiano; kuimarisha ushirikiano katika uchumi, biashara, nishati na mawasiliano; na kudumisha kwa pamoja usalama na uthabiti wa minyororo ya viwanda na ugavi.

Kwa upande wake Mishustin amesema mikutano miwili iliyofanikiwa kati ya Rais Putin na Rais Xi mwaka huu imedhihirisha nia thabiti ya Russia na China ya kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati wa uratibu, na kwamba Russia iko tayari kushirikiana na China kutekeleza kwa dhati makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu hao wawili.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha