

Lugha Nyingine
Upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu nchini DRC waongezwa siku baada ya matatizo ya vifaa na malalamiko
![]() |
Wapiga kura wakiangalia taarifa nje ya kituo cha kupigia kura huko Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Desemba 20, 2023. (Str/Xinhua) |
KINSHASA - Upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utaendelea leo Alhamisi, ametangaza Denis Kadima, Mkuu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) siku ya Jumatano jioni akisema vituo vya kupigia kura ambavyo havikufunguliwa siku hiyo ya jana vitafunguliwa leo Alhamisi.
Wapiga kura takriban milioni 44 nchini DRC walitarajiwa kupiga kura siku ya Jumatano kumchagua rais mpya, wabunge wa Bunge la Taifa na Mabaraza ya Majimbo, pamoja na madiwani wa manispaa, huku kukiwa na ucheleweshaji wa kupeleka vifaa vya kupigia kura na ripoti za ghasia za hapa na pale katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Wapiga kura walipaswa kupiga kura zao siku hiyo kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, lakini kote nchini humo, vituo vingi vya kupigia kura vilikumbwa na matatizo ya vifaa ya kusababisha mchakato wa uchaguzi kutofanyika. Baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa huku foleni ndefu za watu wakingoja.
Wagombea watano wa nafasi ya urais, akiwemo Martin Fayulu na Denis Mukwege, washidani wakuu kutoka upinzani, walitaka kupangwa upya kwa uchaguzi huo ndani ya muda uliopangwa kuamuliwa na washikadau na ofisi mpya ya CENI. Wagombea hawa wamekataa kutambua upigaji kura uliofanyika Jumatano.
Mbali na ubovu wa mashine za kupigia kura, vituo kadhaa pia vilikabiliwa na uhaba wa karatasi na maboksi ya kupigia kura. Baadhi ya wapiga kura waligundua kuwa majina yao hayamo kwenye orodha.
Kwa mujibu wa ujumbe wa uangalizi wa Baraza la Taifa la Maaskofu wa Kongo (CENCO) na Kanisa la Kristo nchini Kongo (ECC), asilimia 31.37 ya vituo vya kupigia kura havikufunguliwa kwa wakati nchini kote.
Wagombea kadhaa wa urais wa upinzani wamepinga hadharani mchakato huo wa uchaguzi unaoendelea.
"Ni machafuko makubwa. Hakuna mpangilio," Martin Fayulu amesema wakati akiondoka kwenye kituo cha kupigia kura mapema siku hiyo baada ya kupiga kura. "Kama kuna vituo vya kupigia kura ambavyo watu hawapigi kura, hatutakubali uchaguzi huu."
Wagombea 26 wamesajiliwa na CENI kushindana katika uchaguzi wa urais, akiwemo Rais aliyeko madarakani sasa Felix Tshisekedi, ambaye anawania kuchaguliwa tena.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma