Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uturuki yaidhinisha ombi la Sweden kujiunga na NATO (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 27, 2023
Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uturuki yaidhinisha ombi la Sweden kujiunga na NATO
Wajumbe wa kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Uturuki wakihudhuria mkutano kuhusu ombi la Sweden kujiunga na Jumuiya ya NATO mjini Ankara, Uturuki, Desemba 26, 2023. (Picha na Mustafa Kaya/Xinhua)

ANKARA - Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uturuki imeidhinisha ombi la Sweden kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) siku ya Jumanne baada ya kujadiliwa, ikiwa ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea kwenye upigaji kura wa bunge kamili ambapo mswada kuhusu kuidhinishwa kwa itifaki ya Sweden kujiunga na NATO umepitishwa na kamati hiyo kwa kupigiwa kura na chama tawala cha Haki na Maendeleo, Chama cha Nationalist Movement, na chama kikuu cha upinzani cha Republican People's.

Chama cha IYI (Good) kimepiga kura ya kupinga mswada huo, ilhali chama cha Peoples' Equality and Democracy hakikushiriki katika upigaji kura.

Fuat Oktay, mwenyekiti wa kamati hiyo, amesema kuwa Sweden imepiga hatua, hasa kuhusu ufadhili kwa ugaidi, lakini ameongeza kuwa Uturuki "bado haijaona matokeo yanayotarajiwa katika vita dhidi ya ugaidi."

Bunge huenda likajadili ombi hilo kwenye mjadala wake mkuu baadaye wiki hii kwa ajili ya kupigiwa kura ya mwisho. Lakini kama bunge litaingia kwenye mapumziko, upigaji kura utacheleweshwa hadi mwaka mpya ujao.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitia saini itifaki ya Sweden kujiunga na NATO na kuiwasilisha bungeni mwezi Oktoba.

Uturuki iliidhinisha ombi la Finland kujiunga na NATO Mwezi Machi lakini imekuwa ikienda polepole kupitisha ombi la Sweden, ikitaka nchi hiyo ya Nordic kushughulikia zaidi wasiwasi wa usalama wa Ankara.

Uturuki iko chini ya shinikizo kutoka Marekani kuidhinisha Sweden kujiunga na NATO, lakini Ankara imekuwa ikizuia uidhinishaji wake ili kuishinikiza Washington kuruhusu uuzaji wa ndege za kivita za F-16 kwa nchi hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha