

Lugha Nyingine
Hamas yasitisha mazungumzo na Israel baada ya naibu kiongozi wa kundi hilo kuuawa Beirut, Lebanon (2)
GAZA/BEIRUT – Kundi la Hamas limetangaza kusitishwa kwa mazungumzo ya kusimamisha vita na Israel katika Ukanda wa Gaza baada ya naibu mkuu wa kundi hilo, Saleh al-Arouri, kuuawa Jumanne jioni katika shambulizi la droni la Israel nchini Lebanon, chanzo cha habari ndani ya Palestina kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
"Tumewafahamisha ndugu wa Qatar na Misri kuhusu kusitishwa kwa mazungumzo," kimesema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina. Qatar na Misri zimekuwa zikipatanisha makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa Kundi la Hamas, lilikataa mazungumzo yoyote kuhusu kufikia makubaliano ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza huku Israel inaongeza uchochezi vita na "mipango ya mauaji" dhidi ya viongozi wa Palestina.
Hapo awali, chanzo cha habari ndani ya Kundi la Hamas kililiambia Xinhua kwamba wasaidizi kadhaa wa al-Arouri, naibu mkuu wa ofisi ya siasa ya Kundi la Hamas, pia waliuawa katika shambulizi hilo la Israel lililolenga ofisi ya Hamas katika kitongoji cha kusini cha mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Katika taarifa yake, Kundi la Hamas limethibitisha kuwa wanachama wake saba wameuawa katika shambulizi hilo la Israel, na kulielezea kuwa ni kitendo cha kigaidi cha "kinyama na cha kutisha", ambacho kinakiuka mamlaka ya kujitawala ya Lebanon, na Israel inapanua uvamizi wake dhidi ya Palestina na watu wake.
Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah la Lebanon limesema shambulizi hilo ni mashambulizi makubwa kwa watu, usalama na mamlaka ya Lebanon.
"Uhalifu huu hautapita bila kulipiziwa na adhabu," limesema katika taarifa, likionya kwamba shambulizi hilo limeashiria "maendeleo hatari" katika mgogoro wa sasa kati ya Israel na Hamas.
Hadi habari hii inachapishwa, hakukuwa na majibu ya mara moja kutoka kwa Israel kuhusu tukio hilo, lakini vyombo vya habari vya Israel, vikiwanukuu maafisa waandamizi, wamesema kuwa nchi hiyo iko katika hali ya tahadhari dhidi ya "kulipiza kisasi" kwa Hamas au mshirika wake anayeungwa mkono na Iran, Hezbollah, ikiwa ni pamoja na kurushwa kwa silaha za kulenga kwa usahihi katika miji ya Israel.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma