Israel yasema muda wa kufikia suluhu ya kidiplomasia na Hezbollah ni "mfupi" huku vifo mjini Gaza vikifikia 22,438

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 05, 2024
Israel yasema muda wa kufikia suluhu ya kidiplomasia na Hezbollah ni
Moshi ukifuka baada ya shambulizi la anga la Israeli mjini Khiam, Lebanon, Januari 4, 2024. (Picha na Taher Abu Hamdan/Xinhua)

JERUSALEM - Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema siku ya Alhamisi kwamba muda wa kufikia suluhu ya kidiplomasia na Kundi la Hezbollah ni mfupi wakati ambapo Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza siku hiyo kuwa idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza imeongezeka na kufikia 22,438 tangu mgogoro kati ya Israel na Kundi la Hamas ulipozuka Oktoba 7, 2023.

Gallant amezungumza hayo mjini Tel Aviv alipokutana na Mshauri Mkuu wa Marekani Amos Hochstein ambaye aliwasili nchini Israel mapema siku hiyo kwa nia ya kupunguza uhasama kati ya Israel na kundi la Hazbollah.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Israel imesema kwenye mkutano na Gallant na maafisa wengine waandamizi wa kijeshi, mjumbe huyo wa Marekani alifahamishwa kuhusu hali ya usalama kwenye mpaka wa kaskazini wa Israel na masharti yanayowekwa na wizara ya ulinzi ya kuwezesha Waisraeli zaidi ya 80,000 waliokimbia makazi yao kurejea nyumbani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) siku ya Alhamisi, jeshi hilo liliendelea kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya Hezbollah Kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo ya kulenga shabaha yalihusisha maeneo ya kurusha roketi, kituo cha uangalizi, na miundombinu mingine ya kundi hilo.

Gazeti la Jerusalem Post limeripoti Alhamisi kwamba katika wiki tatu hadi nne zilizopita, IDF imeanza kulishambulia kundi la Hezbollah "kwa ukali zaidi na kwa upana."

Katika taarifa ya vifo vya Wapalestina, Msemaji wa Wizara ya afya ya Palestina Ashraf al-Qedra amesema kwamba jeshi la Israel limewaua Wapalestina 125 na kujeruhi wengine 318 katika Ukanda wa Gaza ndani ya muda wa saa 24 zilizopita, idadi ambayo inafanya jumla ya vifo kufikia 22,438 na majeruhi kufikia 57,614, huku asilimia 70 ya waathirika ni watoto na wanawake.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha