Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kijiji nchini China walenga kuimarisha uhusiano wa kimataifa na ustawi wa watu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 08, 2024
Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kijiji nchini China walenga kuimarisha uhusiano wa kimataifa na ustawi wa watu
Picha hii iliyopigwa angani Juni 23, 2023 ikionyesha Ligi Kuu ya Kijiji ya China katika Wilaya ya Rongjiang, Mkoa wa Guizhou, Kusini Magharibi mwa China. (Picha na Wang Bingzhen/Xinhua)

GUIYANG -Msimu mpya uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Kijiji ya China (Village Super League), ambayo pia inaitwa "Cun Chao", umeanza Jumamosi katika Wilaya ya Rongjiang, Mkoa wa Guizhou, Kusini-Magharibi mwa China ambapo kwa mujibu wa waandaaji, timu 62 zimesajiliwa kushiriki mashindano ya mwaka huu, ambayo hatua yake ya awali itafanyika kuanzia Januari 6 hadi Februari 24, na fainali zitafanyika Machi hadi Mei.

Mwaka 2023 ligi hiyo, iliyoshirikisha timu 20, ilivutia sana nchini China na duniani kote kwa umaarufu wake, kukidhi mahitaji ya watu wenyeji na hali ya shamrashamra zake.

Ligi hiyo hata ilifuatiliwa na Ligi Kuu ya England, ambayo wawakilishi wake walitembelea Rongjiang na kutoa mafunzo kwa makocha wenyeji.

"Nafikiri Cun Chao ni safi sana, na nimehisi shauku kubwa ya wenyeji kwa soka hapa Rongjiang," Graham Robinson, mshauri wa kimataifa wa Ligi Kuu ya England alisema.

Msimu mpya

He Yun, mtalii kutoka Mji wa Chongqing, Kusini-Magharibi mwa China, alikuja Rongjiang wakati wa majira ya joto mwaka jana kwaajili ya Cun Chao na hajarejea katika mji wake tangu wakati huo. "Sikuwa naelewa soka lakini nilivutiwa na mapenzi ya wenyeji kwake. Ninapenda mazingira haya na ninatazamia msimu mpya," amesema.

Katika msimu wa mwaka huu, timu zimegawanywa katika makundi kumi kwenye hatua ya awali, huku mbili za juu katika kila kundi zikiwania ubingwa wa jumla katika fainali hizo.

Mabadilishano ya Kimataifa

Kwa mapenzi yaleyale ya soka, Septemba mwaka jana, Ligi Kuu ya Soka ya Kijiji ya China na Ligi Kuu ya England zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China.

Desemba 2023, Ligi Kuu ya England ilizindua mradi wa Ujuzi wa Ligi Kuu katika wilaya hiyo ya Rongjiang ili kusaidia kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa soka wenyeji. Warren Leat, meneja wa maendeleo ya soka wa Kituo cha utamaduni cha Uingereza aliendesha programu ya mafunzo ya siku nne kwa makocha 44 ambao pia walicheza kwenye ligi hiyo.

Njia ya kuelekea ustawi

Katika mwaka uliopita, Cun Chao ilipokea maoni zaidi ya bilioni 58 kwenye kurasa zake za mtandaoni. Kuanzia Mei 13 hadi Oktoba 28, Wilaya ya Rongjiang ilivutia watalii zaidi ya milioni 5.19, na kuingiza mapato ya utalii ya yuan bilioni 5.99 (sawa na dola za Kimarekani milioni 843.6).

Shughuli za michezo zinazoshamiri pia zimehamasisha maendeleo ya tasnia husika kama vile bidhaa za batiki zinazouzwa, zikiwemo fulana, mifuko ya kitambaa na nembo za timu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha