

Lugha Nyingine
Blinken ajadili mgogoro wa Gaza na maafisa wa Israeli wakati ambapo WHO imeonya uwepo wa hali mbaya ya kibinadamu (3)
![]() |
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant (Kushoto, kati) akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Tel Aviv, Israel, Januari 9, 2024. (Elad Malka/MoD / Xinhua) |
TEL AVIV - Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amezungumza na maafisa wa Israel mjini Tel Aviv siku ya Jumanne kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Kundi la Hamas na kuitaka Israel kuwalinda raia huko Gaza wakati ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwepo janga la kibinadamu na afya katika ukanda huo siku hiyo huku msaada wa kibinadamu na upatikanaji wa huduma za matibabu ukiendelea kupungua.
Ziara ya Blinken inaashiria safari yake ya nne nchini Israel tangu kuzuka kwa vita kati ya Israel na Kundi la Hamas mwezi Oktoba mwaka jana. Jumuiya ya kimataifa inazidi kuwa na wasiwasi kuhusu mashambulizi ya Israel huko Gaza, kwani idadi ya vifo katika eneo la Palestina imepita 23,000 na watu takriban milioni 2 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na msukomsuko mkubwa wa kibinadamu.
Mgogoro huo umefanya watu milioni 1.9 kuyahama makazi yao, ambayo ni asilimia 85 ya wakazi wote wa Gaza, na kuacha raia katika eneo lililodhibitiwa la Palestina katika hatari ya njaa na magonjwa, limesema Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo pia limesema limenyimwa ufikiaji wa kaskazini mwa Gaza kwa wiki mbili na lililazimika kufuta safari sita za kimatibabu zilizopangwa.
"Hospitali zinafungwa, wagonjwa wanakosa huduma za vituo vya afya, wahudumu wa afya wanalazimika kukimbia kwa ajili ya usalama," Sean Casey, mratibu wa timu za dharura za WHO amesema.
Katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Blinken amesisitiza "umuhimu wa kuepuka madhara zaidi kwa raia na kulinda miundombinu ya raia huko Gaza," kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.
Pia amesisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa haki ya Israel ya kuzuia mashambulizi ya Oktoba 7 yasijirudie tena.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Blinken amesisitiza haja ya kuhakikisha amani ya kudumu na ya endelevu kwa Israel na kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na kutambua nchi huru ya Palestina.
Blinken aliwasili Israel siku ya Jumanne baada ya kutembelea Uturuki, Ugiriki, Jordan, Qatar, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia. Leo Jumatano, atasafiri hadi Ramallah katika Ukingo wa Magharibi kukutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kabla ya kuondoka kuelekea Cairo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma