China na Maldives zapandisha hadhi ya uhusiano wao kwenye mazungumzo ya marais wa nchi hizo mbili

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 11, 2024
China na Maldives zapandisha hadhi ya uhusiano wao kwenye mazungumzo ya marais wa nchi hizo mbili
Rais Xi Jinping wa China na mkewe Peng Liyuan wakifanya hafla ya kuwakaribisha Rais wa Jamhuri ya Maldives Mohamed Muizzu na mkewe Sajidha Mohamed kwenye Ukumbi wa Kaskazini wa Jumba la Mikutano ya Umma kabla ya mazungumzo kati ya Xi na Muizzu mjini Beijing, China, Januari 10, 2024. (Xinhua/Huang Jingwen)

BEIJING - Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Maldives Mohamed Muizzu mjini Beijing siku ya Jumatano ambapo marais hao wawili wa nchi wametangaza kuinua hadhi ya uhusiano wa pande mbili kuwa wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote.

Kwenye mazungumzo hayo, Rais Xi amesema kuwa watu wa nchi hizo mbili walianzisha uhusiano wa kirafiki kupitia njia ya Hariri ya Baharini kuanzia zama za kale, wamefanya ushirikiano wenye mafanikio katika ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na maeneo mengine katika miaka ya hivi karibuni, na kuweka mfano mzuri wa kutendeana kwa usawa, kusaidiana na kunufaishana kati ya nchi kubwa na ndogo katika miaka 52 iliyopita tangu zianzishe uhusiano wa kidiplomasia.

"Katika mazingira mapya, uhusiano kati ya China na Maldives unakabiliwa na fursa ya kihistoria ya kusonga mbele kwa kufuata nyayo", Rais Xi amesema, huku akisisitiza kuwa kuinua hadhi ya uhusiano kunalingana na mahitaji ya maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili na matarajio ya watu wa nchi hizo mbili.

Rais Xi amesema China ingependa kubadilishana uzoefu wa utawala bora na Maldives, kuimarisha muunganisho wa mikakati ya maendeleo, kuhimiza ujenzi wa pamoja wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, na kuweka alama mpya za mafanikio kwenye urafiki kati ya China na Maldives.

Ametoa wito kwa pande hizo mbili kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi, biashara na uwekezaji, maeneo maalum ya kilimo na uchumi wa buluu, kijani na kidijitali, pamoja na kupanuliwa kwa ushirikiano juu ya ulinzi wa ikolojia na mazingira ya baharini, na kuimarishwa kwa mawasiliano kati ya watu katika nyanja za utamaduni.

Kwa upande wake Muizzu amesema anajisikia heshima sana kufanya ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini China akiwa na mawaziri kadhaa muhimu wa baraza la mawaziri na kuwa mkuu wa kwanza wa nchi ya nje kukaribishwa na China mwaka huu, hali inayoonyesha vya kutosha umuhimu mkubwa ambao pande zote mbili zinaweka katika maendeleo ya uhusiano wa pande mbili.

Muizzu amesema Maldives inafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja. Kuungana mkono kithabiti kwa pande zote katika kulinda mamlaka ya nchi, uhuru na ukamilifu wa ardhi, kwani huu ni msingi imara wa maendeleo endelevu na madhubuti ya uhusiano wa Maldives na China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha